Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Dkt. Charles Kichere, amewasilisha
ripoti yake ya mwaka wa fedha 2023/2024 kwa Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu
Hassan Ikulu Jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine amesema
Shirika la Reli Tanzania (TRC) lilipata hasara ya shilingi bilioni 224
ikilinganishwa na hasara ya shilingi bilioni 102 mwaka uliopita.
“Shirika la
Reli Tanzania (TRC) lilipata hasara ya shilingi bilioni 224 ikilinganishwa na
hasara ya shilingi bilioni 102 mwaka uliopita, hasara hii ilichangiwa na
kupungua kwa mapato ya usafirishaji kutokana na uhaba wa vichwa vya treni na
mabehewa pamoja na mvua kubwa iliyosababisha kufungwa kwa njia kwa miezi
minne,” amesema Dkt. Kichere.
Ameongeza kwa
kusema kwamba “Shirika lilitumia shilingi bilioni 29.01 ikiwa ni ruzuku kutoka
Serikalini, kama ruzuku hii isingetolewa Shirika lingepata hasara jumla ya
shilingi bilioni 253.”
Dkt. Kichere
amefafanua kwamba taarifa hiyo inahusu kipindi kinachoishia June 30, 2024 kabla
ya kuanza kutumika kwa treni za SGR kwa hiyo mapato ya SGR hayapo humo.
Pia Dkt.
Kichere akatoa ushauri kwa TRC ijikite katika kuboresha ufanisi wa utendaji
kazi wake ili kuongeza ukusanyaji wa mapato na kutekeleza hatua madhubuti za
kupunguza gharama, iandae mpango wa kina wa kupata injini za treni na mabehewa
ili kukidhi mahitaji ya usafirishaji ipasavyo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2023/24 kutoka Bw. Charles Kichere kwenye hafla fupi iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 27 Machi, 2025.
0 Maoni