Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imetoa
maelekezo kwa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kuendelea kusimamia
miradi ya miundombinu ya utalii inayotekelezwa
ndani Hifadhi ya Taifa Saadani ili kurahisisha watalii kufika kwa urahisi,
kuchochea shughuli za kiutalii na kuongeza mapato ya Serikali.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Japheti Hasunga (Mb),
alitoa maelekezo hayo leo Machi 26, 2025, wakati wa ukaguzi wa miradi miwili
inayotekelezwa ndani ya hifadhi hiyo ikiwemo uboreshaji wa barabara za ndani ya
hifadhi na upanuzi wa uwanja wa ndege.
“Tumeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya miundombinu
inayotekelezwa katika Hifadhi ya Taifa Saadani, sasa endeleeni kusimamia miradi
hii ili kuhakikisha inakamilika kwa viwango vya juu na kuleta manufaa kwa sekta
ya utalii. Pia, tunashauri uwekezaji zaidi katika miundombinu mingine kama
hoteli na huduma za usafiri ndani ya hifadhi ili kuvutia wageni wengi zaidi.”
Alisema Mhe. Hasunga.
Aidha, Mhe. Hasunga alipongeza Menejimenti ya Wizara ya
Maliasili na Utalii, Bodi ya Wadhamini TANAPA na Menejimenti ya Shirika kwa
kufanikisha ongezeko kubwa la mapato ya hifadhi hiyo, ambapo mapato ya watalii
wanaotembelea hifadhi kwa njia ya ndege
yameongezeka kufikia shilingi bilioni 1.68 kuanzia Julai hadi Machi
mwaka wa fedha 2024/2025 sawa na ongezeko la asilimia 19 ikilinganishwa na
makadirio ya ukusanyaji wa kiasi cha shilingi bilioni 1.41 katika kipindi cha
miezi 8.
Vilevile, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini TANAPA, Jenerali
(Mstaafu) George Waitara, alitoa pongezi kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuidhinisha fedha za kutekeleza
miradi hiyo na kuongeza kuwa Serikali imeonesha dhamira ya dhati ya kuendeleza
sekta ya utalii nchini.
“Mhe. Rais amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa miradi
ya maendeleo katika Hifadhi za Taifa inatekelezwa kwa ufanisi. Hatua hii ni
muhimu kwa mustakabali wa utalii nchini, na tunapaswa kuendelea kuwekeza zaidi
ili kuvutia watalii wengi na kukuza uchumi wa Taifa,” alisema Jenerali Waitara.
Naye, Kamishna wa Uhifadhi Shirika la Hifadhi za Taifa
Tanzania (TANAPA), Musa Juma Kuji alieleza kuwa maboresho ya miundombinu ya
utalii Saadani yameongeza mvuto wa hifadhi kwa watalii, hali inayosaidia
kuongeza idadi ya watalii na mapato.
Pia, alibainisha kuwa miundombinu bora huongeza ufanisi wa utoaji huduma
kwa watalii hivyo kuimarisha shughuli za
utalii.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo, Afisa Uhifadhi
Mkuu Gladys Ng'umbi, Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Saadani, alieleza kuwa
maboresho ya miundombinu hiyo yamezingatia viwango vya kimataifa ili
kuhakikisha uwanja wa ndege wa Saadani unakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege
nyingi na kubwa zaidi.
“Maboresho ya uwanja huu yamezingatia viwango vya Mamlaka ya
Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) ili kuhakikisha kuwa uwanja wa ndege wa Saadani
unakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege kubwa zenye uwezo wa kubeba watalii 35 hadi
40 kwa ndege moja ambapo uboreshaji huo utasaidia kuongezeka kwa idadi ya
watalii wanaokuja kutembelea hifadhi pamoja na ongezeko la mapato yatokanayo na
shughuli za utalii,” alisema Ng’umbi.
Hifadhi ya Taifa ya Saadani imekuwa ikifanya maboresho ya
miundombinu ya hifadhi ili kuimarisha shughuli za uhifadhi na utalii
ikizingatiwa kuwa hifadhi hiyo ni muhimu kiikolojia kwani inakutanisha nyika na
bahari katika ukanda wa pwani ya Afrika mashariki.
Na: Zainabu Ally - Saadani
0 Maoni