Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameilekeza Wakala wa Nishati
Vijijini (REA) kutoa ruzuku kwa Jeshi la Magereza ili kutekeleza maelekezo ya
Serikali kuhusu matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na kuhakikisha Magereza
yote yanaondokana na Nishati isiyo safi.
Dkt. Biteko
ametoa agizo hilo leo Machi 28, 2025 jijini Dar es salaam katika hafla ya
kufunga Mafunzo ya Uongozi Ngazi ya Juu Namba 27 - 2024/2025 katika Chuo cha
Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCTA).
“Magereza
yote 129 yamehama katika matumizi ya kuni na sasa yanatumia nishati safi ya
kupikia. Naielekeza REA ile ruzuku tunayopanga kuitoa kwa wazalishaji
mbalimbali kwa ajili ya vifaa vya matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia Magereza
wapewe kipaumbele,” amesema Dkt. Biteko.
Amewapongeza
wahitimu hao wa Mafunzo ya Uongozi Ngazi ya Juu
Namba 27 - 2024/2025 na kusema kuwa ni mategemeo ya Serikali na jamii
kuona wanakuwa chachu ya mabadiliko katika utendaji kazi na kuimarisha
mshikamano katika Jeshi la Magereza.
“Mkuu wa Chuo
ametuthibitishia kuwa mmefanya vizuri katika mafunzo yenu. Na mmekidhi vigezo
vya kupandishwa cheo na Mamlaka husika kuwa Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la
Magereza. Hongereni sana kwa hatua hii kubwa, pamoja na pongezi hizi naomba
niwakumbishe kupandishwa cheo ni kuongezewa majukumu,” ameeleza Dkt. Biteko.
Pamoja na
hayo amewataka wahitimu hao kuwasikiliza na kuwatendea haki kwa askari walio
chini yao sambamba na kuwawajibisha wavivu na kuwatia moyo wachapakazi.
Vilevile,
Dkt. Biteko ametoa rai kwa wahitimu hao kujiendeleza kielimu na kufanya kazi
kwa bidii ili Jeshi la Magereza kuwa la mfano na kutoa huduma bora kwa
Watanzania ili kufikia matarajio ya Serikali.
“Kamishna wa Jeshi la Magereza endelea
kuwaunganisha na kuweka pamoja askari, Serikali inatambua kazi unayofanya na
mchango wako kwa Taifa, Serikali inatambua mchango wa Chuo hiki kwa askari wote”,
amesema Dkt. Biteko.
Akizungumzia
Haki Jinai, Dkt. Biteko amesema “ Niuombe uongozi wa Jeshi, kuendelea na
jitihada za kuboresha utendaji kazi ndani ya Jeshi katika nyanja mbalimbali na
utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Rais ya Kuboresha Haki Jinai ili
kulifanya Jeshi liendane na wakati kwa kuzingatia mabadiliko ya sayansi na
teknolojia.”
Katika hatua
nyingine, Dkt. Biteko amechangia mabati 300 kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi
wa darasa katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania.
Makamu
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Mhe. Vicent Mbogo amempongeza Mhe. Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha vyombo
vya usalama ikiwemo Magereza. Pia amempongeza Mkuu wa Magereza kwa kuwa na
ubunifu wa kuwapeleka wafungwa katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) ambapo huwasaidia
kupata ujuzi mbalimbali.
Akizungumza
kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe.
Edward Mpogolo amemshukuru Mkuu wa Jeshi la Magereza, Kamishna Jenerali
Jeremiah Katungu kwa kusaidia mkoa wa Dar es salaam kuendelea kuwa salama.
“
Tunamshukuru Kamishna Jenerali kwa mchango mkubwa anaoutoa katika mkoa wetu
wakati wa shughuli mbalimbali, hata Maafisa hawa waliohitimu leo wamekuwa na
mchango katika kusaidia usalama wa Mkoa huu,” amesema Mhe. Mpogolo.
Mkuu wa Jeshi
la Magereza, Kamishna Jenerali Jeremiah Katungu amesema hali ya magereza nchini
ni shwari na kuwa Jeshi hilo limeendelea kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki
Jinai.
Amesema
Magereza 66 yana huduma za Mahakama Mtandao na kuwa tayari wamepokea shilingi
milioni 668.8 kwa ajili ya kujenga Magereza Mtandao katika Magereza yote nchini
ili kusaidia upatikanaji haki kwa wakati.
“ Nawashukuru
na kuwapongeza wahitimu wote, utendaji wenu wa kazi uakisi yale yote
mliyojifunza katika nyanja mbalimbali na Jeshi halitaacha kuchukua kwa yeyote
atakayekiuka,” amesema Kamishna Jenerali Katungu.
Mkuu wa Chuo
cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCTA), SACP Wilnton Kahumuza amesema
Mafunzo hayo ya Uongozi Ngazi ya Juu Na. 27 yalianza Novemba 30, 2024
yakiwa na idadi ya wanafunzi 203.
Ameendelea
kusema Mafunzo hayo yalilenga kuwapatia wanafunzi ujuzi mbalimbali ili kuleta
ufanisi katika utekelezaji wa majukumu
mbalimbali ndani ya Jeshi kwa kadri itakavyohitajika.
“Wahitimu
wanaohitimu leo wamefanya mafunzo ya darasani na wanastahili kupandishwa cheo
kwa masomo waliyosomea,” amesema SACP Kahumuza.
Pia,
amewashukuru wahitimu hao kwa kuonesha
kujituma na kuwa na moyo wa kuchanga fedha shilingi 7,703,200 kwa ajili
ya kujenga mnara wa tenki la maji na kununua tenki lenye ujazo wa lita 5,000.
0 Maoni