Waziri wa
Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) amesema kuwa jamii
zimeendelea kunufaika na biashara ya hewa ukaa kupitia miradi ya Shirika la Uhifadhi wa mazingira la ‘The Nature
Conservancy’ nchini Tanzania lililojikita katika kuhifadhi mifumo ya ikolojia ,
kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuongeza mapato kwa jamii.
Ameyasema
hayo katika hafla ya kuwashukuru wadau na kukuza mahusiano na washirika wa
taasisi hiyo iliyofanyika jana Machi 27, 2025 jijini Arusha.
“Tunashukuru
sana kwa msaada wa The Nature Conservancy, hasa kwa kushirikiana na Carbon
Tanzania, kuanzisha miradi ya kaboni katika maeneo muhimu kama vile Yaeda
Chini, Makame Wildlife Management Area (WMA), Ntakata, na misitu ya Tongwe.
Ushirikiano huu sio tu unasaidia kulinda mifumo muhimu ya ikolojia lakini pia
hutoa fursa muhimu kwa jamii za wenyeji kufaidika kupitia mbinu bunifu za
uhifadhi na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi” amesema Mhe.Chana.
Amefafanua
kuwa kupitia biashara ya kaboni Msitu wa Ntakata ulio chini ya Serikali ya
vijiji, wilaya ya Tanganyika, umeingiza dola milioni 24 katika mapato kwa jamii
tangu Juni 2019 na kwamba Carbon Tanzania inaendelea kuhakikisha jamii katika
vijiji 8 inapata dola milioni 12 kila mwaka (takribani tzs bilioni 3 hadi 4
kila mwaka).
Mhe. Chana
ameitaka taasisi hiyo kuendelea kuhakikisha inafanya kazi karibu zaidi na jamii
ili zifaidike na miradi hiyo.
Aidha,
amesisitiza taasisi hiyo kushirikiana na Serikali hasa katika kujenga na
kuandaa maabara ya kisasa katika Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori
Afrika-MWEKA.
“Kituo hiki
kitaboresha sayansi ya uhifadhi, kutoa mafunzo kwa vitendo katika maeneo kama
vile kutambua kwa mbali, baiolojia ya molekuli, sayansi ya mimea/herbariamu, na
kemia ya mazingira. Kwa kuandaa kizazi kijacho cha viongozi wa uhifadhi na zana
hizi za hali ya juu, tunalenga kuunga mkono utafiti unaotumika ambao unaweza
kufuatilia mikopo ya bioanuwai, kuchanganua viwango vya uchafuzi wa mazingira
katika mazingira yetu ya mijini na kando ya miji, na kuchangia juhudi za
uhifadhi wa bahari na utafiti wa jamii,” amesema Mhe. Chana.
Kwa upande
wake Mkurugenzi Mkuu wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Nature Conservancy,
Ademola Adjagbe amesema kuwa Shirika
hilo linafanya kazi katika nchi zaidi ya 80 duniani katika kukabiliana na
changamoto mbalimbali za uhifadhi wa mazingira.
Ameongeza
kuwa Afrika inakabiliwa na changamoto mbalimbali za kimazingira zinazopelekea
upotevu wa rasilimali hivyo ni vyema kushirikiana kuhakikisha Maliasili
zinaokolewa, maisha ya binadamu yanalindwa, kukabiliana na changamoto za
mabadiliko ya tabianchi na kutunza baioanuwai.
Hafla hiyo
imehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Shirika la The Nature Conservancy’s,
wadau mbalimbali wa uhifadhi kutoka Serikalini na Sekta Binafsi.
Na. Happiness
Shayo- Arusha
0 Maoni