Serikali inataka faida itokanayo na uwekezaji ‘return on investment’ katika kampuni ambazo inaumiliki wa hisa chache kuongezeka kutoka asilimia saba ya sasa hadi kufikia zaidi ya 10 mwaka ujao wa fedha
Dhamira hiyo
ilielezwa jana Ijumaa, Machi 28, 2025, na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi
Dkt. Moses Kusiluka wilayani Kibaha, mkoani Pwani, wakati wa kufunga mkutano wa
siku tatu wa wakurugenzi wa bodi za kampuni ambazo serikali inaumiliki wa hisa
chache.
“Niwape
changamoto ya kukuza faida ya uwekezaji kutoka asilimia saba ya sasa kwenda
zaidi ya asilimia 10 kwa mwaka. Na ili kufikia azma hii mnapaswa kuongeza ufanisi wa
utendaji," alisema.
Ofisi ya
Msajili wa Hazina inasimamia jumla ya taasisi 308 ambapo kati ya hizo 56 ni
zile ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache.
Jumla ya
uwekezaji wa Sh86.3 trilioni umefanywa katika taasisi hizo, huku kati ya kiasi
hicho Sh2.9 trilioni zikiwekezwa kwenye kampuni ambazo serikali ina umiliki wa
hisa chache na Sh83.4 trilioni kikienda kwa taasisi ambazo serikali ina umiliki
wa asilimia 100.
Aidha, Balozi
Kusiluka aliwapa changamoto wakurugenzi wa bodi za kampuni ambazo ina hisa chache kuongeza
ufanisi gawio kwa serikali.
“Ninaamini
mwaka ujao wa fedha nitaona gawio kutoka Taasisi mnazosimamia likiongezeka.
Hiyo ni changamoto ninayowaachia,” alisema wakati wa mkutano ulioandaliwa na
Ofisi ya Msajili wa Hazina
Kwa mwaka wa fedha uliopita, serikali ilipata
gawio la Sh195 bilioni kutoka kampuni zake ambazo ina umiliki wa hisa chache,
kwa mujibu wa takwimu kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina.
“Mafanikio
yetu yataakisi juhudi za Serikali chini ya Mhe. Dr. Samia Suluhu Hassan, Rais
wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, ambazo zimekuwa zikifanyika za kuweka
mazingira rafiki na wezeshi ya biashara,” alisema Dk Kusiluka.
Alionesha
imani yake kwa mwongozo ulioboreshwa wa Wakurugenzi wa Bodi wa Hisa chache
uliozinduliwa Jumatano wiki hii wakati wa ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika
katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere.
“Nimeupitia kwa kina na nimeona umejaa mingozo
mizuri itakayotusaidia kutekeleza majukumu yetu kwa weledi na kwa wakati,”
alisema Dk. Kusiluka, huku akiipongeza Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa
kutengeneza Mwongozo huo.
Ni katika
muktadha huo aliwaelekeza wakurugenzi wa bodi kuutumia kikamilifu ili kuongeza
ufanisi katika maeneo yao.
Kwa upande
wake Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Mchechu aliwataka wawakilishi wa serikali
kwenye bodi za kampuni ambazo ina umiliki wa hisa chache kupeperusha vyema
bendera ya Tanzania.
Aliwataka
wawakilishi hao ambao ni wakurugenzi wa bodi kuzitendee haki nafasi walizopewa
ili kuhakikisha kuwa serikali inanufaika na uwekezaji iliofanya kwenye kampuni
ambazo ina umiliki wa hisa chache.
“Nyie ni
jicho la serikali hivyo mnapaswa kutokuchukulia kiwepesi nafasi mlizopewa,
vinginevyo mtakuwa hamuitendei haki serikali na watanzania wote kwa ujumla,”
Bw. Mchechu aliwaambia wakurugenzi hao.
Aliongeza:
“Lazima mjidhatiti na kama unaona hauko kwenye nafasi ya kufanya hivyo kutokana
na kutokuwa na muda wa kutosha, ni vyema ukasema ili nafasi hiyo wapewe
wengine.”
0 Maoni