Kampeni ya kutangaza vivutio vya utalii kupitia Msafara wa
mawakala 30 wa utalii katika bara la Ulaya ijulikanayo kama "My Tanzania
Roadshow 2025' imehitimishwa tarehe 14 Machi 2025 katika Jijini Manchester
nchini Uingereza.
Kampeni hiyo iliyojumuisha
miji mitano iliyoko nchi nne za Ulaya ambayo ni Cologne (Ujerumani),
Antwerp (Ubelgiji), Amsterdam (Uholanzi), London na Manchester (nchini
Uingereza) imekuwa na mafanikio makubwa ambapo waandaaji wamefanikiwa kuvuka
lengo la kuvutia Wakala au Wanunuzi wa Utalii kutoka Tanzania ambapo katika
miji hiyo mitano zaidi ya Mawakala 240
wa nchi za Ulaya walihudhuria mikutano ya kibiashara baina yao na Wakala wa
Utalii 30 kutoka Tanzania.
Mkurugenzi wa Masoko wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Bw.
Ernest Mwamwaja ameeleza kuwa katika
kila mji mikutano hiyo imetoa fursa kwa Wakala wa Utalii wa Ulaya kupata
taarifa za kutosha toka kwa taasisi za uhifadhi zilizoko chini ya Wizara ya
Maliasili na Utalii ambazo ni TTB, NCAA na
TANAPA.
Ushiriki wa taasisi hizi umesaidia kutoa taarifa ya vivutio
vilivyopo na kuelezea uboreshaji wa miundombinu ya utalii, mikakati ya Serikali
ya utangazaji utalii, mwenendo wa utalii, juhudi za Serikali kuongeza mazao ya
utalii, ubora wa huduma, na fursa za uwekezaji zilipo katika sekta ya utalii.
Mawakala wa Utalii kutoka Tanzania wameeleza kuridhishwa na
kiwango cha ueledi katika maandalizi ya kampeni hiyo na ubora wa Wakala
wanunuzi walioalikwa kukutana na Wakala toka Tanzania na kupanua soko la kupata
wateja wa bara la ulaya.
Katika hatua nyingine, Bw. Mwamwaja amezishukuru ofisi za
balozi za Tanzania katika nchi ya Ujerumani, Ubelgiji, Uholanzi, na Uingereza
kwa kuwa chachu ya mafanikio ya Kampeni hiyo na kuwataka Wakala walioko
Tanzania kuendelea kuhudhuria midafara hiyo kila mwaka kuchangamkia fursa
zinazoletwa na Serikali pamoja na sekta binafsi katika kuitangaza Tanzania
katika masoko ya ndani na ya kimataifa.
Akihitimisha msafara huo Bw. Mwamwaja amemshukuru kipekee
Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maono na
juhudi zake binafsi za kutangaza Tanzania katika masoko ya kimkakati ya
kimataifa.
Msafara kutangaza Utalii wa Tanzania My Roadshow 2025 umeratibiwa na Kampuni ya KiliFair ambapo ulianza tarehe 9- 14 Machi, 2025.



0 Maoni