WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea na
mkakati wa kufungua milango ya ujasiriamali kwa kutekeleza sera na programu
mbalimbali zitakazowasaidia wananchi kuendana na soko la ajira ili kujiongezea
kipato.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi Machi 13, 2025) alipoweka
jiwe la msingi la ujenzi wa shule ya Amali ya Makomelo iliyopo Nzega mkoani
Tabora ambayo ujenzi wake umegharimu shilingi bilioni 1.6 .
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali iliamua kutenga
kiasi cha shilingi bilioni 44.7 kwa ajili ya ujenzi shule za amali katika kila
mkoa ili kuwawezesha Watanzania kupata elimu ya mafunzo maalum yatayowasaidia
kujiajiri au kuajiri wengine na hatimaye kujikwamua kiuchumi.
“Lengo letu ni kupanua na kuboresha mazingira ya kujifunzia
na kufundishia sambamba na kutoa elimu yenye ujuzi na vitendo vyenye kukidhi
katika ulimwengu wa ajira.”
“Malengo ya Serikali ni kuwafikisha vijana kupata ujuzi ili
ujuzi huo utumike katika kujipatia kipato na kukabiliana na changamoto ya
ukosefu wa ajira nchini, na bahati nzuri sera yetu ya elimu imesisitiza elimu
ya ufundi mahiri na tunaita amali.”
Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Ofisi ya Waziri
Mkuu iliendesha mafunzo ya ufundi mahiri kwa vijana wenye uhitaji kwenye fani
mbalimbali kwa kuwapeleka kwenye vyuo vikiwemo vya sekta binafsi ili kuwafanya
wawe mahiri kwenye maeneo wanayoona yanaweza kuwaongezea kipato.
“Kwenye elimu tumefanya maboresho ya sera na tumegundua kuwa
vijana wengi nchini wamemaliza ngazi mbalimbali za elimu na Serikali
tunawajibika kuwatafutia fursa za kujiendeleza ikiwemo na vipaji vyao tukaamua
kufanya tafiti ili kufahamu nini tufanye kwa pamoja kukabiliana na tatizo la
ajira”
“Baada ya kufanya tafiti ya namna ya kuboresha eneo la ajira kwa vijana,ambapo vijana wenyewe walishirikishwa na sehemu kubwa ya maoni yao walishauri kujikita kwenye ufundi mahiri kwa kuanzisha mafunzo maalum ya ufundi kwenye ngazi mbalimbali.”


0 Maoni