Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii
imeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
Tanzania (TAWA) ya ujenzi wa barabara (km 30) kwa gharama za shilingi milioni
256 pamoja na ujenzi wa bwawa kwa gharama ya shilingi milioni 125 katika
Hifadhi ya Wanyamapori Makuyuni iliyopo Wilayani Monduli Mkoani Arusha ikiwa ni
mojawapo ya maboresho katika kuendeleza uhifadhi, kukuza utalii na uwekezaji.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili
na Utalii, Mhe.Timotheo Mnzava ameyasema hayo leo Machi 13,2025 wakati wa ziara
ya kamati hiyo ya kukagua miradi hiyo Mkoani Arusha.
"Kipekee tuwapongeze TAWA wanafanya kazi nzuri hasa
katika kazi ya ukarabati na ufunguaji wa barabara na kazi ya utengenezaji wa bwawa,”
amesisitiza Mhe.Mnzava.
Aidha, Mhe. Mnzava ametoa wito kwa Menejimenti ya TAWA
kuendelea kuitangaza hifadhi hiyo ili malengo yaliyokusudiwa, kutatua migogoro
ya mipaka na kujenga mahusiano mazuri na jamii inayozunguka hifadhi hiyo.
Katika hatua nyingine Mhe. Mnzava amesema matamanio ya
kamati hiyo ni kuiona TAWA inaendelea kubuni na kuwaza vyanzo vingine vya
mapato ili iweze kujiendesha bila kutegemea fedha kutoka Serikali kuu.
Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt.Pindi
Chana (Mb) ameishukuru kamati hiyo kwa
maelekezo inayoyatoa mara kwa mara kwa Wizara yake ambapo amesisitiza kupitia
maekezo hayo Wizara ya Maliasili na
Utalii imeweza kutekeleza na kuisimamia vizuri TAWA.
" Tunashukuru kwa maelekezo ya kamati lakini napenda
kuielekeza TAWA hakikisheni hakuna migogoro ya mipaka na wakati umefika wa
kulinda misitu yetu kwa sayansi na teknolojia mfano kwq kutumia kamera za
kisasa, drones ili kuepusha uvamizi na ujangili," Mhe. Chana amesisitiza.
Pia, Mhe. Chana ametia mkazo suala la TAWA kujitangaza huku
akiitaka Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kuhakikisha hifadhi hiyo inatangazwa
ipasavyo ili kuvutia watalii.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na
Utalii (anayeshughulikia Maliasili) CP Benedict Wakulyamba amesema kuwa Wizara
inaendelea na mikakati mbalimbali ya kukabiliana na wanyamapori wakali na
waharibifu kwa kuchimba mabwawa, uongezaji wa vituo vya askari na kutumia
teknolojia mbalimbali.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii iko Mkoani Arusha kwa ziara ya kikazi.




0 Maoni