WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya wasimamie vema fedha za ununuzi wa dawa zinazotolewa na Serikali na kuhakikisha zahanati na vituo vyote vya afya vina dawa za kutosha ili kukidhi mahitaji ya wananchi.
Amesema Serikali
inatenga fedha nyingi kwa ajili ya ununuzi wa dawa muhimu kote nchini hivyo
hatarajii kuona mwananchi anakwenda kupata huduma kisha anaambiwa akanunue dawa
kwenye maduka yaliyoko nje ya vituo vya afya au zahanati.
Ameyasema
hayo alipokuwa akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika
(Machi 25, 2025) katika uwanja wa Shule ya Sekondari Kiraweni, Tarafa ya
Usangi, wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro akiwa katika ziara ya siku moja ya
kukagua miradi wilayani humo.
"Sitarajii
mwana-Mwanga ameenda zahanati, kituo cha afya au hospitali ya Wilaya
anaandikiwa cheti na mganga, halafu unamwambia nenda kwenye duka la mtu binafsi
ukanunue, wakati dawa hiyo inapatikana kituoni hapo.”
Amesema
Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya ununuzi wa dawa kila miezi mitatu
kwenye maeneo yote nchini na hivyo hakuna sababu ya wananchi kukosa dawa
wanapokwenda kupata huduma katika vituo vya Serikali.
"Naomba
niwahakikishie wananchi kwamba fanyeni kazi zenu na muwe na amani kabisa;
katika sekta ya afya Serikali yenu imedhamiria kuimarisha afya zenu mfanye
shughuli mkiwa na matumaini kuwa maeneo ya kutolea huduma yapo."
"Mheshimiwa
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ana maelekezo thabiti kwenye maeneo mbalimbali,
ameelekeza tuimarishe maeneo yote ya kutolea huduma huko huko kwa
wananchi."
Kadhalika,
Mheshimiwa Majaliwa amewataka viongozi wa Halmashauri watenge fedha
zinazotokana na mapato ya ndani kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya
maendeleo ikiwemo ya ujenzi wa zahanati kwenye vijiji. "Nimewaagiza,
fanyeni tathmini ya umbali kutoka kijiji hadi kijiji, na wapi tuanzie. Nenda
mjenge zahanati kimkakati ili tumalize kazi hiyo."
Waziri Mkuu
alihitimisha ziara yake ya siku moja wilayani Mwanga kwa kuwasihi wananchi
kuendelea kuwa na imani na Serikali yao na kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea
maendeleo. “Endeleeni kuiamini Serikali yenu kwani iko imara na itaendelea
kuwahudumia na kuwatumikia,” amesisitiza.
0 Maoni