Wajumbe 85
kutoka nchi 15 za Afrika ambao ni Wajumbe Baraza la Amani na Usalama la Umoja
wa Afrika waliokuwa jijini Arusha kwenye mafunzo ya wajumbe wapya wa
baraza hilo wametembelea eneo la hifadhi
ya Ngorongoro na kustajabishwa na uzuri wa hifadhi hiyo iliyosheheni vivutio
mbalimbali vya utalii.
Balozi wa
Uganda Nchini Ethiopia Mhe. Rebecca Mugotengo ameipongeza Serikali ya Tanzania
kwa juhudi za uhifadhi na ulinzi wa rasilimali za wanyamapori na malikale hali iliyowafanya wajumbe wa mkutano huo kuamua kutembelea
vivutio vya utalii vilivyopo Ngorongoro kabla ya kurudi kwenye nchi zao.
“Wajumbe wa
baraza baada ya kikao chetu Arusha tumechagua kuja Ngorongoro, tumekutana na
watu wakarimu, Ngorongoro ni eneo lenye uoto wa asili lililotunzwa vizuri,
mtawanyiko wa wanyamapori, ndege walioipamba hifadhi, Wanyama ni wengi siwezi
hata kuzungumzia idadi yao, hali hii inawavutia wageni wengi kutembelea eneo
hili” ameeleza Mhe. Rebecca.
Migel Mtutumu
kutoka Nigeria ameeleza kuwa “lUNESCO haikukosea kuitambua hifadhi ya
Ngorongoro kama eneo la urithi wa dunia kutokana na vivutio mbalimbali
vilivyopo.
Amesema
katika muda wa saa tatu waliotumia
katika hifadhi hiyo wameona
Wanyama mbalimbali ikiwepo Wanyama wakubwa watano ambao ni Faru, Chui,
Simba, Nyati na tembo”
Naye balozi
wa Botswana Nchini Ethiopia Mhe. Tibelelo Alfred amepongeza hifadhi ya
Ngorongoro kuwa moja ya kivutio bora cha Utalii Afrika na kubainisha kuwa
wananchi wa Afrika hawahitaji kupeleka fedha katika nchi za ulaya na kuacha
vivutio adhimu ambavyo tunavyo katika bara la Afrika ambavyo vimekuwa kimbilio
la wananchi wa mataifa mbalimbali.
Kiongozi wa
Ujumbe huo ambaye ni Balozi wa Tanzania Nchini Ethiopia na
Mwakilishi wa kudumu katika Umoja wa Afrika Mhe. Innocent Eugine Shio ameeleza
kuwa wajumbe wa baraza hilo baada ya kumaliza programu ya mafunzo ya siku mbili
jijini Arusha waliamua kuwaandalia ziara ya kutembelea hifadhi ya Ngorongoro
waweze kujionea uzuri wa Ngorongoro na waliowengi imekuwa mara yao ya kwanza kuona
idadi kubwa ya Wanyama wakiwa katika mazingira ya asili ikiwemo Wanyama wakubwa
watano “Big 5” na kuahidi kurudi mara nyingine
wakiwa na familia zao.
Na. Kassim
Nyaki - NCAA
0 Maoni