Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Kanali Ahmed Abbas Ahmed,
ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa uratibu mzuri wa Tamasha la
Kumbukizi la Vita vya Majimaji, linalofanyika kila mwaka katika mkoa huo kwa
lengo la kuwaenzi mashujaa wa vita hivyo.
Akizungumza jana katika maadhimisho
ya Siku ya Wangoni (Ngoni Day) yaliyofanyika Kijiji cha Maposeni, Kanali Ahmed
amesema kuwa siku hiyo ni mwendelezo wa matukio kuelekea kilele cha kumbukizi
ya mashujaa waliopoteza maisha yao katika harakati za kupinga utawala wa
kikoloni wa Kijerumani.
Amesema uratibu wa tamasha hilo umeendelea kuwa wa kiwango
cha juu kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa pamoja na Baraza la Mila na
Desturi. Mafanikio haya yanadhihirika kwa mwitikio mkubwa wa wananchi, jambo
linaloonesha uzalendo na heshima kwa mashujaa wetu, alisema Kanali Ahmed.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kumbukizi hizo kuwa ni njia ya kuwaenzi mashujaa 67 waliopoteza
maisha yao wakipigania uhuru wa Taifa.
“Leo tupo hapa tukifurahia matunda ya amani, rasilimali,
mila na tamaduni zetu. Haya yote ni matokeo ya kujitolea kwa mashujaa wetu,
hivyo ni muhimu kuendelea kuwaenzi kwa vitendo,"alisisitiza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Malikale na
Makumbusho kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. William Mwita alieleza
kuwa wizara itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha tamasha la
kumbukizi ya mashujaa wa Vita vya Majimaji linaendelea kuimarika na kuwa chachu
ya uzalendo kwa Watanzania.
“Uwepo wa Makumbusho ya Majimaji ni darasa muhimu kwa Taifa
letu katika kuhifadhi historia na urithi wa kihistoria. Ni wajibu wetu kulinda
rasilimali zetu na kuzihifadhi kwa kizazi cha sasa na kijacho,"alisema
Mwita.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi wa Ruvuma kujitokeza kwa wingi kushiriki katika kilele cha maadhimisho ya kumbukizi hizi, kama walivyoshiriki kwa hamasa kubwa katika mashindano ya ngoma za asili, kongamano la kihistoria, na maadhimisho ya Siku ya Wangoni.
Na. Said Lufune - Ruvuma
0 Maoni