Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Jenerali Jacob John
Mkunda amesema Maadhimisho y Miaka 120 ya kumbukizi ya Vita vya Majimaji
inapaswa kutumika kama kielezo na somo tosha la ulinzi wa rasilimali za taifa
zilizopo hapa nchini.
Jenerali Mkunda amesema
hayo leo Februari 27, 2025 Mkoani Ruvuma akifunga tamasha la kumbukizi la vita
vya Majimaji vilivyoanzia kusini mwa Tangangika mnano mwaka 1905 hadi 1907
ambapo amesema roho za mashujaa hao zitaendelea kuwa mbegu kutokana na moyo na
uzalendo wa kulipigania Taifa lao.
“Watu hawa hawakua majambazi wala wavamizi bali ni watu
waliojitolea kuulinda uhuru wao, utamaduni wao, heshima yao na rasilimali zao
huku wakijua fika silaha zao zikiwa duni kuliko za wavamizi, lakini moyo wao
wakizalendo uliwapa nguvu ya kusimama kwa pamoja na kupinga ukoloni hadi tone
la mwisho,” amefafanua Jenarali Mkunda.
Aidha, amewataka
wananchi kujiepusha na uvivu, ubadhilifu wa mali za umma, matumizi ya dawa za
kulevya na rushwa kwa kuwa kufanya hivyo ni kusaliti roho za mashujaa wa taifa
hili na badala yake kutumia fursa zilizopo katika kufanya kazi kwa bidii ili
kujipatia kipato na kuchangia ukuaji wa uchumi na pato la taifa.
‘‘Nitumie fursa hii kuipongeza Serikali ya awamu ya sita
chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
kwa kutoa msukumo wa pekee kwenye sekta ya utalii nchini na kuufanya uchumi
wetu kukua kwa asilimia 24.3 hadi kufikia mwaka 2023 na kuchangia kukua kwa
pato la ndani kwa asilimia 17.2 kupitia sekta ya utalii,’’ amesema.
Katika hatua nyingine Jenerali Mkunda amempongeza Waziri wa
maliasili na Utalii Mhe. Balozi. Dkt.
Pindi Chana kwa kuitangaza vyema sera ya utalii ndani na nje ya nchi.
Ameutaka uongozi wa Mkoa wa Ruvuma kuunga mkono juhudi hizo
kwa kufanya utafiti wa kubaini vivutio vipya vya Urithi wa Makumbo na Malikale
ili kuongeza chachu katika ukuaji wa uchumi.
Akiongea kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na
Utalii Mkurugenzi Msaidizi wa Malikale na Makumbusho kutoka Wizara hiyo Bw. William Mwita amesema kuwa pamoja na
kuadhimishwa kwa kumbukizi za mashujaa hao Wizara inaendelea na mikakati ya ya
kuhifadhi wa makumbusho ya Majimaji kwa kushirikiana na wadau katika kubaini
maeneo yaliyotumika wakati wa vita vya Majimaji na kuyatangaza kuingia katika orodha ya urithi wa Taifa.
“Lengo ni kuhakikisha kuwa historia hii haishii tu kuwa
kumbukumbu ya Taifa, bali pia inakuwa chachu ya utalii wa utamaduni,
unaochangia katika maendeleo ya jamii na pato la jamii za mikoa ya kusini mwa
Tanzania na Taifa kwa ujumla,” amesema
Mwita.
Mwita amesisitiza kuwa Wizara hiyo inaendelea na jitihada za kukusanya na kuhifadhi mikusanyo inayohusiana na vita ya Majimaji na kuyahifadhi Makumbusho ya Majimaji katika mkoa hua ili kutumika kama sehemu ya kujifunza, utafiti na vivutio kwa watalii kutoka ndani na nje ya nchi.
Na. Saidi Lufune - Ruvuma
0 Maoni