Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema ujio wa Watafiti wa Mimea Vamizi kutoka nchini Cuba waliokuja nchini watasaidia katika kukabili Mimea Vamizi katika Hifadhi ya Taifa Saanane pamoja na Ziwa Viktoria ambayo yamekuwa changamoto katika Shughuli za usafirishaji, Uvuvi na Utalii.
Mhe. Mtanda amebainisha hayo leo Februari 24, 2025 mara
baada ya kuipokea timu ya Watafiti wa Mimea vamizi kutoka Jamhuri ya Cuba
walioungana na Wataalamu wa Ikolojia kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii ambao
wametembelea mwambao wa Ziwa Viktoria eneo la Kigongo Busisi pamoja na Hifadhi
ya Taifa Kisiwa cha Saa Nane ambapo amesema ujio wa wao utaleta suluhu ya
tatizo la Magugu ya maji katika Ziwa hilo kubwa na katika Hifadhi hiyo ya
kipekee Duniania.
"Tumefurahi kupata huu ugeni wa Watafiti wa Mimea
Vamizi kutoka Cuba, ambao wameandaliwa kuja na Wizara ya Mambo ya Nje kupitia
Balozi wetu wa Tanzania Mhe. Balozi. Humphrey Polepole na Wizara ya Maliasili
na Utalii kwani wamekuja wakati muafaka kwakuwa hivi karibuni kuna gugu vamizi
linazaa mara kwa mara na kwa muda mfupi ziwa limekuwa linafunikwa kwahiyo
huathiri miundombinu ya usafirishaji na samaki wa Vizimba," alieleza Mkuu
wa Mkoa Mtanda.
Aidha, ameeleza kuwa Magugu vamizi yanaweza kuleta athari
kwa wafugaji wa Samaki kwa njia ya vizimba hivyo serikali imeleta wataalamu hao
katika muda muafaka.
“Sasa hivi Ziwa Viktoria tunafuga samaki kwa vizimba na kuna
vizimba takribani 1047, kwahiyo endapo gugu vamizi litaendelea kusambaa katika
maeneo mengine litaleta athari kiuchumi, kwa vijana wafugaji ndio maana
tunaishukuru serikali kwa kuwaleta Wataalamu haraka kabla hawajaathirika,” aliongeza
Mhe. Mtanda.
Afisa Mistu Mkuu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii ambaye
pia ni Mwenyekiti ziara ya timu ya watafiti mimea vamizi kutoka Jamhuri ya Cuba
na Tanzania Bw. Emmanuel Msofe amasema sekta mbalimbali zimeathiriwa na Mimea
Vamizi hususani katika maeneo yaliyohifadhiwa kisheria hivyo ziara ya Watafiti
hao inatarajiwa kuleta neema katika Mkoa wa Mwanza na Tanzania kwa ujumla.
Naye Kaimu Mkuu Hifadhi ya Kisiwa cha Saa Nane Afisa
Mhifadhi Mkuu Pellagy Marandu ameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kukuza
sekta ya utalii ikiwemo kuleta Watafiti hao ambao watakuwa msaada mkubwa katika
kutatua tatizo hilo ambalo limekuwa kero
ya mara kwa mara katika mageti ya kuingilia Hifadhini na kutoka.
Timu ya Watafiti wa Mimea vamizi kutoka Jamhuri ya Cuba walioungana na Wataalamu wa Ikolojia kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii inatarajiwa kuleta suluhu ya tatizo la mimea vamizi katika maeneo yaliyohifadhiwa pamoja vyanzo vya maji kwa lengo la kuleta ustawi wa sekta mbalimbali zinazoathiriwa nachangamoto hiyo.




0 Maoni