Wahenga
walisema isiyo kongwe haivushi, lakini leo Kilwa imetuvusha. Hayawi hayawi
yamekuwa, leo Tanzania inathibitisha yale yaliyosemwa na wahenga miongo kadhaa
pale mji wa kihistoria wenye historia ya kipevu mji wa Kilwa Mkoani Lindi
unaposhuhudia mpishano wa meli kubwa za kifahari za Kitalii zilizosheheni
watalii kutoka pembe za dunia zikishusha mamia ya watalii katika Hifadhi ya
urithi wa utamaduni wa dunia ya Magofu ya Kale ya Kilwa Kisiwani na Songo
Mnara.
Ilikuwa Februari
09, 2025 majira ya Saa 2 asubuhi katika
bandari ya mji wa Kilwa wahifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori
Tanzania - TAWA na wakazi wa mji huo walipokusanyika kuwalaki wageni kutoka
Mataifa mbalimbali duniani.
Taratibu Meli
kubwa ya viwango vya Kimataifa ijulikanayo Kwa jina la Ponant Le Bougainville
kutoka visiwa vya Seycheles yenye hadhi ya kutia nanga katika bandari ya nchi
yenye utajiri wa vivutio vya utalii, nchi
inayoongozwa na Kiongozi shupavu mwenye maono Mhe. Dkt Samia Suluhu
Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ilianza kushusha watalii mmoja
baada ya mwingine na kufikisha Idadi ya watalii 124.
Bendera za
Mataifa takribani 14, zilionekana zikipepea Kilwa Kisiwani huku wanawake Kwa
wanaume, watoto kwa wakubwa wakizuru sehemu mbalimbali za Hifadhi hiyo ya
kihistoria yenye vivutio vingi vya asili na urithi wa kiutamaduni. Sura za
wageni hao zikionekana kujaa bashasha na shauku ya kujifunza mengi huku majengo
yaliyojengwa kwa ustadi wa ajabu yakichagiza udadisi wao.
Australia,
ubeligiji, Canada, Ufaransa, Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi na New
Zealand ni miongoni mwa Mataifa yaliyotembelea Hifadhi hiyo bila kusahau Ureno,
Shelisheli, Uswisi, Uingereza na Marekani.
Machweo
yalipowadia watalii walianza kuingia ndani ya meli ya kifahari, na taratibu Meli kuanza kutikia huku wageni hao
wakipunga mikono yao Kwa Wakazi wa Kilwa na wahifadhi wa TAWA Hifadhi ya urithi
wa utamaduni wa dunia Magofu ya Kale ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara.
Hii ni Meli
ya 5 ya kitalii kutia nanga Kilwa tangu mwaka 2025 ulipoanza. Mpishano wa meli
hizi kushusha watalii Kilwa ni kielelezo cha mapinduzi makubwa katika Sekta ya
utalii na mabadiliko ya kiuchumi yaliyoletwa na Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
0 Maoni