Shirika la
Kimataifa linalojihusisha na Uhifadhi, Frankfurt Zoological Society (FZS)
limeendelea kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Shirika la Hifadhi za
Taifa Tanzania (TANAPA) katika Uhifadhi wa Maliasili katika Hifadhi za Taifa
Nchini ambapo leo Februari 10, 2025 wamekabidhi gari moja lori aina ya ISUZU
kwa TANAPA chini ya mradi wa Dharura wa Uhifadhi na Utalii Tanzania (Emmergency
and Recovery Support for Biodiversity (ERB).
Akizungumza
katika hafla ya makabidhiano hayo iliyofanyika katika ofisi za TANAPA Makao
Makuu jijini, Arusha, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara
TANAPA, Massana Mwishawa aliipongeza FZS kwa namna ambavyo imekuwa ikisaidia
juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kupitia TANAPA katika Uhifadhi na Utalii.
“Serikali ya
Tanzania kupitia Shirika lake la TANAPA imekuwa na ushirikiano mzuri na
Serikali ya Ujerumani kupitia FZS kwa takribani miaka sitini sasa katika
kuhifadhi kuendeleza jamii. TANAPA tunaamini kwamba hatuwezi kuhifadhi bila
kuigusa jamii, ni lazima jamii inufaike, Hivyo kupatikana kwa gari hili
kutasaidia katika shughuli za Ujirani Mwema katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.”
“Gari hili
litatumika kuchukua vikundi vya kijamii kutoka katika maeneo yao na kuwaleta
katika Hifadhi ya Taifa Serengeti kujifunza shughuli za Uhifadhi na Utalii
lakini pia litatumika kusafirisha kikundi kimoja cha kijamii kwenda kikundi
kingine kwa lengo la kujifunza zaidi,” alisema Kamishna Mwishawa.
Aidha,
Kamishna Mwishawa alimtaka Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti Kamishna Msaidizi
Mwandamizi wa Uhifadhi Stephano Msumi, kuhakikisha gari hilo linaelekezwa
kwenye matumizi stahiki na kuhakikisha kwamba linatunzwa vizuri ili kuleta tija
iliyokusudiwa.
Mkurugenzi
Mkazi wa Shirika la Frunkfurt Zoological Society (FZS), Dkt. Ezekiel Dembe
ameeleza kuwa FZS itaendelea kushirikiana na TANAPA katika kuendeleza juhudi za
Uhifadhi na utunzaji wa Mazingira nchini.
“Lengo letu
ni kuona TANAPA inakwenda mbele zaidi katika Uhifadhi. Tunaahidi ushirikiano
zaidi katika Uhifadhi na Maendeleo ya Hifadhi za Taifa. Hifadhi hizi zinapaswa
kutuzwa vizuri endapo tutaziharibu tufahamu kuwa tumeharibu mazingira, na
mazingira yanayo namna yakutuadhibu na hata vizazi vijavyo vitatulaumu kwa
kutotunza Mazingira vizuri,” alisema Dkt.Dembe.
Andrew
Mwakisu ambaye ni Mratibu wa Mradi wa ERB kutoka FZS alibainisha kuwa mradi huo
umekuwa na manufaa makubwa katika shughuli za Uhifadhi katika Hifadhi ya Taifa
Serengeti, na Nyerere.
“Hifadhi ya
Serengeti kwa kweli imebahatika kupata malori manne ikiwemo mawili kwa shughuli
za kawaida za Uhifadhi, lori moja kwa ajili ya kubeba wanyama na sasa hili
ambalo tunalitoa leo lilikuwa limebakia kati ya yale malori nane likiwa ni
kwaajili ya Ujirani Mwema.”
“Mradi
wa ERB umefanya mambo mengi tumeweza kununua magari na vifaa mbalimbali hili ni
lori la Nane sasa, malori mengine yalikwenda Selous, Nyerere, na Serengeti.
Ikiwa ni mwaka wa mwisho wa mradi huu tumeona ufanisi mkubwa katika maeneo
yanayofaidika na mradi huu”.
FZS
imekabidhi kwa TANAPA lori aina ya ISUZU linaloweza kubeba watu 30 kwa wakati
mmoja likiwa na thamani ya dola za kimarekani 177,966/= linaloenda kutumika na
Idara ya Ujirani Mwema katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Na. Edmund Salaho - Arusha
0 Maoni