Katika kuendelea kupambana na magonjwa yasiyoambukiza
ikiwemo magonjwa ya moyo, shinikizo la
juu la damu pamoja na kisukari, Hospitali ya Taifa Muhimbili Mloganzila inaendelea na kambi maalum ya
upasuaji rekebishi wa kupunguza mafuta katika sehemu mbalimbali za mwili kwa
watu wenye uzito uliopitiliza ili kuwapunguzia athari ya kupata magonjwa hayo.
Daktari Bingwa wa Upasuaji MNH -Mloganzila, Dkt. Eric
Muhumba amesema kambi hiyo inalenga kuwasaidia watu ambao walikuwa wakihangaika
kupunguza uzito kwa njia mbalimbali bila mafanikio.
Ameongeza kuwa pamoja na kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza kambi hiyo pia inalenga kuwasaida baadhi ya watu ambao wamekuwa wakipata maumivu kutokana na baadhi ya viungo vyao vya mwili kuwa vikubwa kupita kiasi na kusababisha kupata maumivu ya mgongo.
Kambi hiyo itakayodumu kwa muda wa siku tano kuanzia Februari 20 hadi 27, 2025 inafanyika
kwa kushirikina na Dkt. Shraddha
Deshpande ambaye ni Bingwa wa Upasuaji Rekebishi kutoka nchini India. Mpaka
sasa jumla ya watu sita wenye uzito uliopitiliza wamefanyiwa upasuaji huo.

0 Maoni