WAZIRI MKUU, Mhe. Kassim Majaliwa amesema jitihada za kujenga mahusiano ya kidiplomasia baina ya Tanzania na nchi washirika zinazofanywa na Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan zimekuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania.
"Tangu aingie madarakani Mheshimiwa Rais Dkt Samia
Suluhu Hassan amekuwa kinara katika kujenga mahusiano na nchi mbalimbali jambo
ambalo limeleta heshima kubwa na manufaa kwa nchi yetu hususan kwa kufungua
fursa za kibiashara na uwekezaji kutoka
nchi washirika."
Ameyasema hayo leo (Jumatatu Februari 24, 2025) alipokutana
na ujumbe wa wabunge wa bunge la Ulaya (EU) kutoka Kamati ya Ushirikiano na
Maendeleo kwenye Ofisi ndogo ya Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar es Salaam.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amebainisha kuwa Umoja wa Ulaya
umeendelea kuwa mdau mkubwa wa Tanzania katika kukuza biashara na uwekezaji
kupitia nchi washirika. "Tanzania inathamini ushirikiano wa kiuchumi na
kidemokrasia uliopo kati ya Tanzania na nchi za Umoja wa Ulaya."
Amesema biashara baina ya Tanzania na nchi washirika wa
Umoja wa Ulaya imeendelea kukua na nchi inanufaika kwa kupokea wawekezaji
kutoka katika umoja huo.
"Uwekezaji wa nchi za Ulaya katika sekta ya kilimo,
nishati, miundombinu, madini na utalii umekuwa kwa kiasi kikubwa. Pongezi
zimwendee Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kufungua milango ya ushirikiano
huu."
Kwa Upande wake, Mjumbe wa Bunge la Ulaya, Mheshimiwa Barry
Andrews ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kazi kubwa inayofanya ya kuboresha
maisha ya wananchi wake zikiwemo sekta
za afya, elimu na miundombinu.
"Tanzania imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa
mikataba mbalimbali ya kimataifa ya maendeleo endelevu, ikiwemo utoaji wa
huduma bora za afya, na elimu kwa wananchi.”
Amesema Umoja wa Ulaya utaendelea kuwa mshirika muhimu wa
maendeleo wa Tanzania katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
"Katika miaka 20 iliyopita Tanzania imepiga hatua kubwa
sana kwenye maboresho ya huduma za jamii na sasa kuna miundombinu bora ya usafirishaji
inayochangia kukua kwa uchumi, Tunawapongeza sana."
Ujumbe huo wa wabunge 14 wa Bunge la Ulaya uko chini Tanzania kwa ziara ya kikazi ya Siku tatu na utakutana na Viongozi wa Serikali wadau wa maendeleo na wanufaika wa miradi inayoungwa mkono na Nchi washirika wa Umoja wa Ulaya.




0 Maoni