Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya
mazungumzo na Waziri wa Petroli na Gesi Asilia wa India, Mhe. Hardeep Singh
kuhusu nia ya nchi hiyo kuzidi kuimarisha biashara kati yake na Tanzania
kupitia sekta binafsi, kufanya uwekezaji kwenye Sekta ya Nishati na kujengea
uwezo wataalam.
Mazungumzo
hayo yamefanyika Februari 11, 2025 jijini New Delhi nchini India katika
Maadhimisho ya Tatu ya Wiki ya Nishati nchini humo.
Dkt. Doto
Biteko amemweleza Waziri Singh kuwa milango ya uwekezaji Tanzania ipo wazi na kampuni mbalimbali kutoka India zinaweza
kuwekeza kwenye maeneo mbalimbali
ikiwemo ya umeme, usambazaji wa gesi ya mitungi (LPG) na uagizaji wa mafuta kwa
pamoja (Bulk procurement) kwani kunahitajika washindani wengi ambao watatoa
uhakika wa uwepo wa mafuta wakati wote.
“Tanzania
tumejikita katika kuhakikisha tunatumia kila rasilimali tuliyonayo ili kuwa na
nishati ya kutosha ikiwemo umeme ili kukidhi mahitaji ya wananchi,” amesema
Dkt. Biteko.
Aidha,
ameeleza kuhusu umuhimu wa ushiriki wa sekta binafsi katika kuendeleza miradi
mbalimbali akitolea mfano kuwa, ili Tanzania ijitosheleza kwa mahitaji ya
nishati inahitaji Dola za Marekani Bilioni 12 ambazo kupatikana kwake lazima
sekta binafsi ihusishwe hivyo kupitia kwa Waziri Singh, amekaribisha wawekezaji
kutoka India kuwekeza kwenye Sekta ya Nishati nchini.
Kuhusu
ushiriki wa Tanzania katika Wiki ya Nishati India amesema kuwa Tanzania
imefaidika na ushiriki wake katika Wiki hiyo kwani India tayari imeshapiga hatua kwenye Sekta ya
Nishati hivyo imekuwa ni sehemu maalum ya kujifunza zaidi kuhusu sekta, kubadilishana
uzoefu na kunadi fursa za uwekezaji ikiwemo duru ya tano ya uendelezaji wa
visima vya mafuta na gesi asilia
Tanzania.
Kwa upande
wake, Waziri wa Petroli na Gesi Asilia wa India, Mhe. Hardeep Singh amesema
kuwa India ina uhusiano mzuri wa kibiashara na Tanzania ambapo biashara kati ya
pande hizo mbili imezidi kuimarika na kueleza kuwa nchi hiyo imejipanga
kuimarisha zaidi biashara yake kwa Tanzania.
Ameeleza
kuwa, nchi hiyo pia kupitia Sekta binafsi inataka kuwekeza kwenye usambazaji wa
mitungi ya gesi nchini hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali inatekeleza
Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati
Safi ya Kupikia huku akieleza kuwa nchi hiyo imepiga hatua kubwa kwa kusambaza
mitungi ya gesi kwa asilimia 99.9 kwa wananchi wake.
Ameongeza
kuwa India imeamua kuwekeza kwenye uendelezaji wa Mafuta na Gesi Asilia ambapo
baadhi ya kampuni zake zimejitokeza kushiriki Duru la Tano la kunadi vitalu vya
Mafuta na Gesi Asilia linalotarajiwa kufanyika mwaka huu mwezi Machi nchini.
“India pia
tupo tayari kuwekeza kwenye gesi ya kusindika (LNG), bayofueli pamoja na
kushirikiana na Tanzania katika masuala ya kitaalam yanayohusu Sekta ya Nishati
kwa kuwajengea uwezo zaidi wataalam wa Tanzania na pia kuwa na programu ya
kubadilishana wataalam kati ya Tanzania na India,” asema Mhe. Singh.
Pia,
ameipongeza Tanzania kwa kupiga hatua kubwa kwenye usambazaji wa umeme hususan
vijijini na kwa jinsi inavyotekeleza mkakati wa nishati safi ya kupikia kwa
namna mbalimbali ikiwemo kuweka ruzuku kwenye mitungi ya gesi.
Vilevile,
Waziri Singh amempongeza pia Dkt. Biteko kwa hekima zake na ukomavu ambao
anauonesha pale anapoieleza dunia kuhusu masuala ya uendelezaji wa rasilimali
zinazoweza kuzalisha umeme ambazo Bara la Afrika imebarikiwa nazo lakini mpaka
sasa hazijaendelezwa ipasavyo kutokana na misimamo ya kidunia ikiwemo makaa ya
mawe ambayo yakiendelezwa yatazidi kutoa
uhakika wa uwepo wa nishati ya kutosha.
Mazungumzo
kati ya viongozi hao yamehudhuriwa pia
na Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambaye
anamwakilisha Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Idd Kassim, Kamishna wa Umeme na
Nishati Jadidifu Mhandisi Innocent Luoga na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Dkt. James Andilile.


0 Maoni