Mmoja wa wamiliki (co-owners) wa vilabu vya michezo vya Manchester United ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), klabu ya soka ya Nice ya Ligi Kuu ya Ufaransa (League 1) na timu ya Marcedes katika mbio za magari za Formular 1, Sir Jim Ratcliffe, ameahidi kushirikiana na Serikali ya Tanzania kuendeleza uhifadhi na kutangaza utalii ili kuhakikisha Tanzania inazidi kunufaika na raslimali ilizonazo.
Sir Ratcliffe ambaye pia ni Mwenyekiti wa makampuni ya
mafuta na gesi ya INEOS, ameyasema hayo kwenye ofisi zake ndogo za mjini
Monaco, Ufaransa, leo Ijumaa Februari 28, 2025, alipokutana na Dkt. Hassan
Abbasi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na ujumbe wake.
Sir Ratcliffe, muumini mkubwa wa masuala ya uhifadhi
duniani, na akiwa anamiliki taasisi yake ya Six Rivers Africa inayosaidia
moundombinu, tafiti na uendelezaji wa uhifadhi na utalii hasa katika maeneo ya
Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania, ameisifu Serikali ya Tanzania chini ya Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio makubwa katika uhifadhi lakini pia na
utalii.
“Huwa nakuja nchini kwenu. Ninatarajia kuja tena Tanzania
mwaka huu. Nitatoa tarehe zangu kuja kuonana na kumpongeza Rais Samia kwa
kuendeleza uhifadhi. Tanzania ndio nchi pekee, kwa maoni yangu, hapa duniani
kwa sasa, iliyowahifadhi wanyama wengi hasa wale wakubwa, maeneo mengi
wametoweka.
“Hata sisi huku Ulaya wala mabara mengine hatuna wanyama
wengi na wakubwa kama mlio nao Tanzania. Tunaahidi kuendelea kushirikiana na
Serikali ya Tanzania kuendelea kuwahifadhi,” alisema Sir Ratcliffe.
Katika mazungumzo hayo Dkt. Abbasi pamoja na kuwasilisha kwa Sir Ratcliffe ujumbe maalum wa Serikali, alimuomba kutumia ushawishi wake wa kuwa na hisa katika klabu na timu mashuhuri za michezo kusaidia juhudi za Rais Samia kutangaza utalii jambo ambalo amelifurahia na kuahidi kulifanyia kazi.
0 Maoni