Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt.
Emmanuel John Nchimbi, amesema kuwa mapambano ya uhuru wa kiuchumi na ustawi wa
kijamii katika nchi za Kusini mwa Afrika yanaendelea kwa kasi kubwa, ikiwa ni
njia ya kuwaenzi waasisi wa ukombozi wa kisiasa katika ukanda huo.
Akizungumza katika tukio la utoaji heshima za mwisho kwa
Rais wa Kwanza wa Namibia na Baba wa Taifa hilo, Mhe. Dkt. Sam Shafiishuna
Nujoma, lililofanyika tarehe 27 Februari 2025 katika Uwanja wa Sam Nujoma,
jijini Windhoek, Balozi Nchimbi alisema kuwa kizazi cha sasa cha viongozi wa
ukanda huo, pamoja na vyama vilivyoongoza harakati za ukombozi, kinaendelea
kuthamini na kuenzi jitihada za waasisi wa uhuru.
Alisisitiza kuwa waasisi hao walijitoa kupigania misingi ya
utu wa binadamu, demokrasia, Umoja wa Afrika, uhuru wa kujitawala, amani, na
mshikamano-misingi ambayo ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya watu wote barani
Afrika na duniani kwa ujumla.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na maelfu ya waombolezaji, wakiwemo
viongozi wakuu wa chama tawala cha Namibia, SWAPO.
Miongoni mwao walikuwa Makamu wa Rais wa SWAPO, Komredi
Netumbo Ndemupelila Nandi Ndaitwah, ambaye pia ni Rais Mteule wa Namibia,
pamoja na Katibu Mkuu wa SWAPO, Komredi Sophia Shaningwa. Familia ya Hayati Sam
Nujoma pia ilihudhuria tukio hilo, sambamba na viongozi wa vyama mbalimbali
rafiki.
Balozi Nchimbi alieleza masikitiko yake kwa kifo cha Mhe.
Dkt. Nujoma, akisema:
“Taarifa za kifo cha Rais Nujoma zilitusikitisha sana.
Tulipopata habari hizi tulishtuka sana. Alikuwa kiongozi pekee aliyebaki hai
miongoni mwa waasisi wa ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika, na mmoja wa
waasisi wa Nchi za Mstari wa Mbele. Alikuwa amana yetu iliyobaki ya hekima na
alama ya ukombozi wetu. Tunahisi kuibiwa. Tunahisi kupotea!”
Akitafakari mchango wa Hayati Dkt. Nujoma katika harakati za
ukombozi wa Kusini mwa Afrika, Balozi Nchimbi alieleza kuwa ushindi wa Namibia
dhidi ya ukoloni ulikuwa wa kimkakati kwa mataifa ya mstari wa mbele. Kupata
uhuru kwa Namibia kulitoa fursa muhimu ya kuendeleza mapambano dhidi ya utawala
wa kibaguzi wa makaburu nchini Afrika Kusini.
“Rais Nujoma ni miongoni mwa viongozi waasisi wa Afrika
waliokomboa nchi zao na wakaachia madaraka kwa hiyari na kidemokrasia. Kwa
kufanya hivyo, aliiweka Namibia kwenye njia sahihi ya demokrasia na uongozi wa
amani. Hilo linaeleza kwa nini Namibia leo hii ni mfano bora wa demokrasia
barani Afrika. Huu ni urithi wake wa kudumu,” aliongeza Balozi Nchimbi.
Akirejea kumbukumbu za harakati za ukombozi wa Afrika,
Balozi Nchimbi alifichua jinsi Mzee Nujoma alivyolazimika kwenda uhamishoni
wakati wa mapambano ya uhuru wa Namibia, akitumia pasipoti ya Tanzania yenye
jina la Samuel Mwakangale. Hii ni ishara ya namna Tanzania ilivyokuwa ngome
salama kwa SWAPO na harakati za ukombozi kwa ujumla.
Balozi Nchimbi pia alinukuu salaam za Mwenyekiti wa CCM na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa
watu wa Namibia, akimwelezea Dkt. Nujoma kama:
“Mpigania uhuru, Mwafrika shupavu, na rafiki wa kweli wa
Tanzania, ambaye aliwahi kuishi hapa wakati wa harakati za ukombozi wa Namibia.
Aliishi maisha ya utumishi, yaliyounda mstakabali na mwelekeo wa nchi yake,
huku akihamasisha vizazi kusimama kwa ajili ya maadili ya uhuru, usawa, na
haki.”
Katika hitimisho lake, Balozi Nchimbi aliwasilisha ujumbe wa
heshima kwa waasisi wa ukombozi wa Afrika waliotangulia mbele za haki:
“Nembo yetu ya mwisho imeondoka. Shujaa wetu wa mwisho
ameanguka. Kiongozi wetu wa mwisho wa nchi za mstari wa mbele ameenda kuungana
na wenzake. Komredi Nujoma, tafadhali tunakuomba utufikishie salaam za heshima
kwa Julius Nyerere, Agostinho Neto, Samora Machel, Kenneth Kaunda, Robert
Mugabe, na Nelson Mandela. Tunawashukuru kwa kutuletea uhuru wa kisiasa.
Waambie kuwa mapambano ya ustawi wa kiuchumi Kusini mwa Afrika yanaendelea!”
Mazishi ya kitaifa ya Hayati Dkt. Sam Nujoma yamepangwa
kufanyika tarehe 1 Machi 2025, katika eneo la makaburi ya mashujaa, jijini
Windhoek, baada ya kuagwa rasmi kitaifa tarehe 28 Februari 2025, ambapo
yakihudhuriwa na viongozi wa ndani na nje ya Namibia.
0 Maoni