Walanguzi wa mazao ya wakulima wa kahawa, mahindi, mbogamboga na karanga wameondoka baada ya kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya Ilolo-Ndolezi yenye urefu wa Km 11.01 kwa kiwango cha lami katika halmashauri ya wilaya ya Mbozi mkoani Songwe.
Wakiongea kwa nyakati tofauti baadhi ya wakazi wa kitongoji
cha Isiniza kijiji cha Mbimba wamesema kuwa barabara hiyo imewarahisishia
kusafirisha mazao yao kutoka mashambani hadi kwenye masoko, hivyo kuwaongezea
kipato.
Bi. Salome Nzunda amesema wanaishukuru serikali kwa
kuwajengea barabara hiyo ambapo zamani ilikuwa na changamoto sana kwani
barabara haikuwa inapitika.
“Zamani tulikuwa tunapita barabara ya kutoka Vwawa kwenda
Ndolezi, ilikuwa na changamoto sana hata mtu akiumwa kwenda hospitali ya wilaya ilikuwa kazi, barabara
ilikuwa haipitiki hata vifo vya wajawazito na watoto vilikuwepo sana.”
“Tulikuwa tunashindwa kupita kwenye barabara hii, ilikuwa
tope haswa na tulikuwa tukitumia hadi saa mbili kwenda mjini, lakini sasa hivi
tunatumia dakika 15 kufika mjini, tunaishukuru serikali wametutengenezea
barabara hii tunaweza kufika hospitali ya wilaya hata ya mkoa na vifo sasa hivi
vimepungua,” aliongeza.
Vile vile amesema kwamba, barabara hiyo imeondoa pia
walanguzi wa mazao yao ambapo awali walanguzi hao walikuwa wakipita kwenye
nyumba zao na kununua mazao kwa bei ya chini, lakini hivi sasa wanasafirisha
wao wenyewe kwenda kuuza kwenye soko kuu la Vwawa mjini, hivyo kuwaongezea
kipato na kuweza kuimarisha maisha yao kwa kujenga nyumba za bati tofauti na
zamani walikuwa na nyumba za nyasi.
Naye, Bw. Heckson Mwambalo mkazi wa kijiji cha Mbimba
amesema kuwa, wananchi wamefurahi sana kwani imewasaidia kusafirisha mazao yao
kwa urahisi.
“Tunaishukuru serikali kwa kutuona na kutujengea barabara
hii kwani njia hii kutoka Vwawa, Idiwili kwenda Ndolezi haikuwa inapitika, mvua
ikinyesha hatukuwa tunafanya chochote tulikuwa tukisubiri jua litoke ndiyo
twende kuchukua mazao kwa kweli wananchi wote tumefurahi.”
Kaimu Meneja wa TARURA mkoa wa Songwe, Mhandisi Lugano
Mwambingu amesema barabara ya Ilolo-Ndolezi imejengwa kupitia mradi wa
Agri-Connect kwa thamani ya Shilingi Bilioni 6.46 na hadi sasa umekamilika kwa
100%.
Amesema barabara hiyo imejengwa kwa kiwango cha lami pia
wamejenga safu za boksi kalavati (3), safu za zege 35 kuweka alama za
barabarani 50, mfereji wa maji ya mvua Km 6.456 pamoja na kuweka taa za
barabarani 40.
Aidha, Mhandisi Mwambingu ameongeza kusema kwamba barabara
hiyo imesaidia kuongeza uzalishaji wa mazao ya biashara pamoja na mpango wa
kurahisisha mawasiliano kwa wananchi wanaoishi katika Kata za Iyula, Idiwili na
Mlangali.
“Barabara hii imekuwa na muhimu sana kwa wakulima wa vijiji
hivi kwani imefungua fursa za kiuchumi katika bonde hilo kwani kila zao
linakubali na kuinua kipato cha mwananchi mmoja mmoja.”
Ameongeza kusema kwamba barabara hiyo imewarahisishia
wakulima kupeleka kahawa yao kiwandani pia mazao mengine kwenye masoko pamoja
na kupeleka katika maghala ya kuhifadhia mazao yaliyopo mjini.
Mkoa wa Songwe unahudumia mtandao wa barabara wa Km. 3,341.628
ambapo barabara za lami Km.36.38, changarawe Km. 1155.718, udongo Km. 2,149.53,
madaraja 212 pamoja na makalavati 1,971.
0 Maoni