Katika kuhakikisha kuwa njaa haichangii watoto wao kufanya
vibaya katika masomo yao, wazazi Shule ya Sekondari ya Muhoji wameridhia kwa
pamoja kuchangia upatikanaji wa chakula cha mchana kwa wanafunzi wote.
Shule hiyo mpya iliyopo katika jimbo la Musomo Vijijini
ambalo kipaumbele chake namba moja ni elimu, wazazi wameonyesha kupata muamko mkubwa
wa elimu, kufuatia jitihada zinazofanywa na mbunge wao Prof. Sospeter Muhongo.
Maamuzi hayo ya wazazi ambayo yanajenga msingi mzuri wa
elimu kwa watoto wao, yamefanyika jana katika kikao ambapo pamoja na mambo
mengine wazazi wamekubaliana kununua madawati ya watoto wao. Madawati
yanatengenezwa kijijini hapo Muhoji.
Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge wa Musoma Vijijini
pamoja na mambo mengine wazazi hao wameahidi watahakikisha kuwa kuna uhusiano
mzuri baina yao na walimu, na kati ya wanafunzi na walimu.
Tayari matayarisho ya ufunguzi wa Shule hiyo mpya ya Muhoji
Sekondari ya Kijijini Muhoji, Kata ya Bugwema, Musoma Vijijini yameanza na
wazazi wameahidi kuendelea kushirikiana vizuri na Serikali kuhakikisha
Sekondari yao inatoa elimu kwenye mazingira mazuri yenye mafanikio.
Jimbo la Musoma Vijijini lenye Kata 21, lina Sekondari za
Kata 26, ambapo mbili ni za binafsi. Sekondari mpya 6 zimepagwa kufunguliwa mwaka huu. Matayarisho
ya kuanza ujenzi wa sekondari nyingine sita yamekamilika.
0 Maoni