Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imeandaa kambi
maalum ya upasuaji wa marejeo (revision) wa kupandikiza nyonga na magoti
kuanzia Februari 26 hadi Machi 07, 2025.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Upasuaji
Dkt. Godlove Mfuko kambi hiyo itafanywa na wataalam wa Muhimbili Mloganzila kwa
kushirikiana na Daktari Bingwa Mbobezi wa Upandikizaji wa Viungo kutoka nchini
China Prof.Tian Hua.
Dkt. Mfuko amebainisha kuwa hospitali imeamua kuanzisha
huduma hizo za marejeo kutokana na uhitaji wa watu wengi wanaokuja kutafuta
huduma hiyo hospitalini hapo na kutofanikiwa hivyo uongozi ukaona ipo haja ya
kuwapunguzia usumbufu wa maumivu na gharama za kutafuta huduma hizi nje ya nchi.
“Serikali imeendelea kuwajengea uwezo wataalam wa ndani
ili kufanya huduma za ubingwa bobezi kama hizi, sasa ni wajibu wetu sisi kama
wataalam kuanzisha huduma mpya kwa lengo la kuwapunguzia gharama na usumbufu
wananchi kwenda kutafuta huduma hizi nje ya nchi. Awali upasuaji huu ulikua
haufanyiki hapa nchini kutokana na upatikanaji wa nyonga na magoti bandia
maalum kwa ajili ya upasuaji wa marejeo pamoja na utaalam,” ameongeza Dkt.
Mfuko.
Dkt. Mfuko amesema kuwa huduma za marejeo za upandikizaji
wa nyonga na magoti hufanyika kutokana na nyonga na magoti yaliyowekwa mwanzo
kusagika au changamoto zingine na kuongeza kuwa kwa wale wanaohitaji huduma
hizi wafike hospitalini mapema kwa uchunguzi na hatimaye matibabu.
Hospitali ya Taifa Muhimbili imefanya huduma za
upandikizaji wa nyonga na magoti kwa zaidi ya wagonjwa 256 tangu huduma hizo
zilipoanza kutolewa hospitalini hapa mwaka 2023.
0 Maoni