Mkuu
wa Wilaya ya Kilombero Mhe. Wakili Dunstan Kyobya amesema Serikali
haitawafumbia macho watu watakaohusika kudhoofisha jitihada za kulinda na
kuhifadhi Pori la Akiba Kilombero
ambalo ni mahsusi Kwa ajili ya kuhifadhi vyanzo vya maji, misitu na
wanyamapori hususani upatikanaji wa maji Kwa ajili ya uzalishaji wa umeme
katika mradi wa kimkakati wa Bwawa la Mwl. Nyerere.
Akizungumzia
umuhimu wa kuhifadhi Hifadhi hiyo Januari 03, 2024 wilayani humo, Mhe. Wakili
Dunstan Kyobya amekemea vikali tabia ya watu wachache wanaowalaghai wananchi
kulima na kuchunga mifugo ndani ya Hifadhi pamoja na kuwauzia maeneo Kwa ajili
ya kilimo.
"Imetokea
tabia ya watu kwenda kuwashawishi wananchi kwamba maeneo ya hifadhi
yanaruhusiwa kulima na kuchunga mifugo, nasema maeneo ya hifadhi hayaruhusiwi
kwa shughuli zozote za kibinadamu isipokuwa zile zinazoruhusiwa kisheria,"
amesema Wakili Kyobya.
"Lakini
kuna wengine wanawatapeli wananchi Kwa kuwauzia maeneo ndani ya Hifadhi,
nimuombe OCD (Mkuu wa Polisi Wilaya)
pamoja na Kamati ya usalama ya wilaya kuendelea kufuatilia kwa ukaribu
na wale wote watakaobainika wanawadanganya wananchi, wanawalaghai, wanawatapeli
Kwa njia moja ama nyingine tutachukua hatua," amesisitiza Mhe. Kyobya.
Aidha,
Mhe. Wakili Kyobya ametoa wito Kwa viongozi wa Wilaya yake kuongeza ulinzi katika
Pori la Akiba Kilombero na kuweka utaratibu mzuri wa kuwapokea wananchi
wanaohama kutoka ndani ya Hifadhi hiyo hasa katika maeneo yaliyo pembezoni mwa
Hifadhi kama vile Mofu, Idete, Mawala, Chombe na Mgeta.
Maeneo
mengine aliyoyataja ni pamoja na Chita, kalengakyelu,Chisano Ching'anda,Mlimba, Utengule na mengine
yanayozunguka hifadhi huku akisisitiza kuwa imani na nia nzuri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan isiharibiwe na watu wachache.
Naye
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mlimba Jamal Idrisa Abdul amemshukuru Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Kwa kulipandisha
hadhi Pori la Akiba Kilombero na kusisitiza kuwa Kazi iliyobaki ni kuhakikisha
Halmashauri Kwa kushirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania -
TAWA wanailinda na kuihifadhi Hifadhi hiyo sambamba na kurejesha uasili wake.
Mkurugenzi
huyo amesema mpaka sasa Kazi kubwa wanayoendelea nayo ni kuhakikisha wananchi
hawaendelezi shughuli za kibinadamu katika Hifadhi hiyo.
Kwa
upande wake Kamanda wa Pori la Akiba Kilombero Bigilamungu Kagoma amesema tangu
Hifadhi hiyo ipandishwe hadhi TAWA imeendelea na zoezi la uwekaji vigingi ili
kuifanya mipaka ya Hifadhi kuonekana na kutambulika vizuri na wananchi ambapo
mpaka sasa zaidi ya vigingi 1,100 tayari vimekwisha wekwa.
Na.
Beatus Maganja - Kilombero
0 Maoni