WANANCHI wa Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara wameishukuru Serikali kwa kuwapelekea mradi wa ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja ambao utasaidia kufungua uchumi wa wilaya hiyo.
Wakizungumza
wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi hiyo wananchi hao wamesema awali kabla ya
ujenzi wa miundombinu hiyo walikuwa wakikumbana na changamoto za usafiri na
usafirishaji bidhaa na mazao mbalimbali yanayolimwa wilayani humo jambo
lililochangia kuzorota kwa ukuaji wa uchumi wao.
Bw.
Jafari Hassan ambaye ni dereva wa bodaboda Mkazi wa Kijiji cha Mbeli katika
Kata ya Mbeli wilayani humo anasema awali alikuwa akikumbana na changamoto
katika shughuli zake za usafirishaji kabla ya kujengwa kwa daraja
linalounganisha kata hiyo na maeneo mengine lakini kwa sasa anafurahia kazi
yake baada ya kujengwa kwa daraja hilo la mawe.
“Kwa
sasa tuna ‘enjoy’, tulipata shida sana kwa kukosekana kwa hili daraja hususani
sisi bodaboda, tulipata changamoto kubwa kusafirisha akina mama kwenda kliniki
mpaka tunaamua kupita ng’ambo lakini kwa sasa tunamshukuru Mungu kwa kupata
daraja zuri kama hili na sasa tunapita juu, kwa kweli daraja hili
limeturahisishia sana tunaishukuru Serikali na viongozi wetu wametukamilishia
daraja ni jambo jema sana,” alisema Jafari.
Naye,
Bw. Bakari Kilama, Mkazi wa Mji mdogo wa Matui wilayani humo anasema hapo awali
hakukuwa na barabara nzuri kiasi ambacho wakazi wa mji huo walikuwa wakipita
kwenye njia ambazo magari yalikuwa yakipasua kwa kupita ndipo na wao wapite
ukilinganisha kwa sasa baada ya kujengewa barabara ya uhakika pamoja na mitaro.
Amesema
kwa kiwango kikubwa shida hiyo imepungua na sasa wanaweza kusafirisha mazao yao
kutoka katika mji huo na kuyapeleka maeneo mengine kwaajili ya biashara jambo
ambalo limewanufaisha kiuchumi.
“Kwanza
zamani hakukuwa na barabara yaani ilikuwa tu watu wanapita kwenye mapalio
ambayo magari yanapasua yenyewe, lakini kwa mradi huu ambao wamekuja
kututengenezea hizi barabara tunashukuru kwa sababu kwa kiwango kikubwa tabu
imepungua ya kusafirisha mazao yetu kutoka hapa kwenda sehemu nyingine, imekuwa
kidogo ni rahisi, kwa hiyo sisi wananchi wa hapa tumenufaika kwa hili,” alisema
Bakari.
Kwa
upande wake Bw. Siraji Ally ambaye ni Mkazi wa Matui anasema amefurahi baada ya
kupelekwa mradi wa barabara mjini humo ambapo hapo nyuma walikuwa wakipata
shida hasa watoto wa shule walikuwa wakishindwa kuhudhuria vipindi vya masomo
kutokana na wingi wa maji yaliyokuwa yakituama jambo lililosababisha kuzorota
kwa elimu katika mji huo lakini kwa sasa baada ya ujenzi wa barabara na mitaro
hali imekuwa shwari.
Siraji
ameipongeza Serikali kupitia Wakala ya Barabara Vijijini na Mijini (Tarura) na
kusema kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo imewarahisishia kusafirisha mazao yao
ikiwemo mahindi, alizeti, karanga na mbaazi baada ya magari kuweza kufika
katika mashamba yao na hivyo kukua kwa mzunguko wa biashara katika mji huo.
“Barabara
ni kitega uchumi, kwa sababu bila barabara maendeleo hakuna, maana yake utatoa
mazao hapa utapeleka sehemu nyingine kama huna barabara nzuri, lakini kama
barabara sio nzuri sio rafiki huwezi kupeleka mazao sehemu nyingine. Kwa hapa
tunashukuru kwa sababu mazao sasa yanatolewa hapa yanapelekwa sehemu nyingine,
kwa hiyo mzunguko wa biashara unakuwepo,” alisema.
Akizungumzia
kuhusu miradi ya Barabara na madaraja wilayani humo Meneja wa Tarura Wilaya ya
KIteto, Mhandisi Edwin Magiri amesema Tarura inahudumia mtandao wa Barabara
wenye jumla ya Kilometa 1,291.137, kati ya hizo Kilometa 200.3 ni changarawe,
Kilometa 5.128 barabara za lami na Kilometa zaidi ya 1,014 ni barabara za
vumbi.
Mhandisi
Magiri amesema anaishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais
Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga Bajeti ya shilingi Bilioni 2.8 kwa mwaka
wa fedha wa 2024/2025 kutoka Bajeti ya shilingi Bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi
na ukarabati wa miundombinu wilayani humo ambayo ni ongezeko la zaidi ya
asilimia 100 na kufanya hali ya upitikaji wa barabara na madaraja wilayani humo
kufikia asilimia 19 kutoka 11 ya awali.
“Katika
kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia
Suluhu Hassan tumejenga zaidi ya madaraja 18, kwa hiyo madaraja ya teknolojia
ya mawe tumeyajenga katika maeneo mbalimbali ambayo gharama zake ni nafuu
kidogo ukilinganisha na yale madaraja ya zege,” alisema na kuongeza.
“Awali
tulikuwa na Bajeti ya Bilioni 1.684 ambayo tulipata kutoka kwenye Mamlaka ya
Serikali za Mitaa, lakini baada ya hapo tukaenda kwenye Bajeti ya Bilioni 1.3
kabla ya awamu ya sita, lakini baada ya awamu ya sita Bajeti ya uhakika ambayo
tunayo ni Bilioni 2.8 kwa hiyo ni ongezeko la zaidi ya silimia 100,” alisema
Mhandisi Magiri.
Aidha,
amesema licha ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu hiyo, lakini pia wanatoa
rai na elimu ya mara kwa mara kwa wananchi wa Kiteto kuhusu kuitunza
miundombinu hiyo ambayo Serikali imetoa fedha nyingi kuijenga ili iweze kudumu
kwa manufaa yao.
0 Maoni