Waziri wa Madini, Mh. Anthony Mavunde (Mb) amesena kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na Italia katika kuendeleza sekta ya madini nchini hususani katika teknolojia na mitambo.
Ameyasema
hayo jana tarehe 06 Januari, 2025 alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi
wa Italia nchini Tanzania, Mh. Giuseppe Coppola katika ofisi ndogo za Wizara ya
Madini Jijini Dar es Salaam.
"Rais
wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameifungua nchi yetu kwa kuimarisha
mahusiano kimataifa kupitia falsafa yake ya 4R. Sisi wasaidizi wake tutaendelea
kuhakikisha tunasimamia maono hayo na kujenga mahusiano zaidi na washirika wetu
kwa manufaa ya uchumi na wananchi wa pande zote”.
Zipo
fursa nyingi kwenye sekta ya madini nchini kuanzia kwenye utafiti mpaka
uongezaji thamani madini, mazingira ya uwekezaji ni mazuri hivyo
ninawakaribisha sana wawekezaji kutoka nchini Italia kuja kuwekeza Tanzania, alisema
Mavunde.
Kwa
upande wake Balozi Coppola, aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano
inaompa tangu awasili nchini, na kusisitiza kwamba Italia inayo makampuni mengi
ambayo yamejikita katika teknolojia hususan utengenezaji wa mitambo inayotumika
kwenye sekta ya madini.
"Mwezi
Februari, 2025 tunataraji kuwa na mkutano wa wafanyabiashara baina ya Tanzania
na Italia ambapo tunatarajia makampuni na wawekezaji katika sekta zote hususan
madini kuja kushiriki mkutano huo. Ninaamini kwa kutumia mkutano huo utakuwa ni
mwanzo mzuri wa wawekezaji kutoka Italia kuona fursa zilizopo nchini Tanzania
na kuanza kuzichangamkia," alisisitiza Mhe. Coppola.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mavunde alionesha kufurahishwa na mpango wa mkutano wa
wafanyabiashara wa Italia na Tanzania na kutanabaisha kwamba ni vizuri taarifa
za kina kuhusu mkutano huo zikaifikia Wizara mapema kwa ajili ya uratibu ili
wachimbaji wakubwa na wadogo waweze kushiriki kikamilifu na kuleta tija.
0 Maoni