Walinzi wa Rais Yoon wazuia polisi kumkamata

 

Jeshi la Korea Kusini likiongozwa na walinzi wa Rais wa nchi hiyo leo limewazuia askari polisi takribani 3000 wasimkamate Rais wa nchi hiyo, Yoon Suk Yeol ambaye ameondolewa madarakani na Bunge hivi karibuni baada ya polisi hao ambao wameambatana na wachunguzi wa masuala ya kupinga rushwa kuzingira makazi ya Yoon wakiwa na kibali cha kumkamata.

Wanasheria wa Yoon wamesema wachunguzi hao wanaojaribu kumkamata Yoon wamevunja sheria kwakuwa hati ya kumkamata ipo kinyume cha sheria na kusema watawachukulia hatua za kisheria polisi na wachunguzi hao kwa kitendo hicho.

Bunge la Korea Kusini lilipiga kura ya kumuondoa Yoon madarakani mwezi Desemba mwaka 2024 baada ya Rais huyo kutangaza sheria ya matumizi ya nguvu ya kijeshi akisema ni kwa ajili ya kulinda nchi yake dhidi ya vitisho vya vikosi vya kikomunisti vya Korea Kaskazini.

Yoon Suk Yeol ameapa kupambana hadi dakika ya mwisho kubaki kwenye kiti chake cha urais licha ya kupigiwa kura ya kuondolewa madarakani ambapo, wafuasi wake wameendelea kupiga kambi katika makazi yake wakizuia Yoon kuhojiwa au kukamatwa.

Wachunguzi wana hadi Januari 6 kumkamata Yoon kabla ya hati ya sasa kuisha. Wanaweza, hata hivyo, kutuma maombi ya hati mpya na kujaribu kumweka kizuizini tena.

Chapisha Maoni

0 Maoni