Polisi mlevi awaachia watuhumiwa washerehekee mwaka mpya

Afisa wa Polisi wa nchini Zambia aliyekuwa amelewa amewaachilia watuhumiwa wa uhalifu 13 kutoka kizuizini ili waende kusherehekea mwaka mpya, maafisa wanasema.

Inspekta wa upelelezi Titus Phiri alikamatwa baada ya kuwaachilia watuhumiwa hao kutoka kituo cha polisi cha Leonard Cheelo katika Mji Mkuu, Lusaka.

Washukiwa hao 13 walishtakiwa kwa makosa ya uhalifu kama vile kushambulia, ujambazi na wizi. kwa sasa wote hawajapatikana na msako umeanzishwa ili kuwatafuta.

Afisa huyo alifungua gereza la wanaume na wanawake na kuwaagiza watuhumiwa waondoke huku akisema wako huru kusherehekea kuingia mwaka mpya.

Taarifa ya polisi inasema, kati ya watuhumiwa 15 waliokuwa kizuizini, 13 walitoroka, na baada ya tukio hilo, afisa huyo alikimbia eneo la tukio, kabla ya kukamatwa.


Chapisha Maoni

0 Maoni