Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) amesema kuimarika kwa
miundombinu ya Mahakama ni hatua muhimu itakayowawezesha wananchi kupata huduma
katika mazingira mazuri, salama na rafiki.
Ameyasema hayo leo Januari 1, 2025 wakati akiweka Jiwe la
Msingi la ujenzi wa Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Magharibi B huko Kisakasaka,
Zanzibar.
Balozi Kombo amesema, kwa miaka mingi mahakama zimekuwa
na changamoto ya miundombinu ya majengo na Serikali inayoongozwa na Dkt.
Hussein Ali Mwinyi imedhamiria kumaliza changamoto hizo kwa kujenga majengo
mapya na ya kisasa.
"Kwa mfano jengo lililokuwa likitumiwa na Mahakama
ya Magharibi B pale Mwanakwerekwe lilikuwa finyu mno kiasi cha kusababisha
msongamano mkubwa na kuwapa usumbufu waliofuata huduma mahali pale,"
alisema Mhe. Kombo.
Waziri huyo ameongeza kuwa, pamoja na ufinyu huo, pia
halikuwa rafiki kutokana na kukosekana nafasi kwa ajili ya maofisa wa Mahakama.
Vilevile, kukosekana kwa huduma za watu wenye mahitaji
maalumu na maegesho kulisababisha muda mwingi wananchi walikuwa wanazagaa kwa
kukosa sehemu tulivu ya kusubiri huduma.
Amesema, hali hiyo ndiyo iliyosababisha Serikali kuchukua
hatua za makusudi kuja na mradi wa ujenzi wa majengo ya Mahakama ya mikoa na
wilaya Unguja na Pemba.
Pia, amesema ujenzi wa jengo hilo ni sehemu ya
utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa majengo saba ambao ulipangwa kufanyika katika
mwaka wa fedha 2023/2024.
Kwa upande wa Unguja, Balozi Kombo amesema, mradi huo wa
Loti Nambari 2 unajumuisha majengo manne ambayo ni: Mahakama ya Mkoa wa
Kaskazini, Mahakama ya Mkoa wa Mjini Magharibi, Mahakama ya Mkoa wa Kusini na
Mahakama ya Wilaya ya Magharibi B.
Serikali inaendelea kuwekeza fedha nyingi katika ujenzi
wa miundombinu ya majengo ya ofisi, hivyo ni wajibu wa watumiaji wa miundombinu
hii na wananchi kwa ujumla kuitunza ili iweze kudumu kwa
miaka mingi ijayo.
0 Maoni