Shangwe la Sikukuu na TANAPA lamfikia Dkt. Gharib Bilal

 

Ikiwa ni msimu wa sikukuu za Krismas na Mwaka mpya 2025, Ujumbe wa Shangwe la Sikukuu na TANAPA umemfikia Makamu wa Rais(Mstaafu) wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Mohamed Gharib Bilal katika Hifadhi ya Taifa Tarangire.

Ujumbe wa Shangwe la Sikukuu na TANAPA umeongozwa na Kamanda wa Uhifadhi Kanda ya Kusini, Steria Ndaga, ambaye amemwakilisha Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, pamoja na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Tarangire Betrice Kessy, na baadhi ya Maafisa wa Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Tarangire.

Mhe. Dkt.Bilal aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Shirika lake la TANAPA kwa namna ambavyo limeboresha miundombinu katika Hifadhi zake ikiwemo Hifadhi ya Taifa Tarangire.

“Serikali kupitia TANAPA mnafanya kazi kubwa nimeona mabadiliko makubwa hapa Tarangire, miundombinu ni ya uhakika, wanyama ni wengi na mazingira ni mazuri sana, nimefurahia sana huduma zenu hapa Tarangire naahidi nitarudi tena hapa,” alisema Mhe. Bilal.

Aidha, Mhe.Bilal alipongeza vijana wa kitanzania kwa kuwa na elimu na maarifa mengi katika maswala ya Utalii na Uhifadhi, maarifa ambayo mengi wameyapata katika vyuo vyetu vya ndani ambayo hutumika kuhudumia wageni wanaotembelea maeneo mbalimbali ya vivutio.

    Na. Edmund Salaho - Tarangire


Chapisha Maoni

0 Maoni