Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam leo Januari 13 imeshindwa
kusikikiza kesi ya kusambaza taarifa za uongo inayomkabili aliyekuwa Katibu Mkuu
wa CHADEMA, Dkt. Wilbroad Slaa (76) kwa sababu ya kutofikishwa mahakamani.
Dkt. Slaa alifikishwa mahakamani hapo Januari 10, 2025
akikabiliwa na kesi ya jinai namba 993 ya mwaka 2025, ambapo alitarajiwa
kufikishwa mahakamani hapo leo kwa ajili ya kujua hatma ya dhamana
yake baada ya upande wa Jamhuri kuwasilisha kiapo cha kuzuia dhamana.
Wakili wa Serikali, Issa Tawabu amesema kuwa kesi hiyo
imeitishwa leo kwa ajili ya mjadala wa dhamana lakini mtuhumiwa hajafika
mahakamani licha kwamba alitakiwa kufika leo na akisisitiza kuwa wameuliza
lakini wameambiwa hajafika.
Kutokana na mvutano wa kutofikishwa mahakamani kwa
mtuhumiwa na hatma ya dhamana yake, huku hoja nyingine zikiibuka kutoka pande
zote mbili za Mawakili wa Serikali na Utetezi, Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki
ameahirisha kesi hiyo hadi Januari 17, 2025.
Dkt. Slaa alifikishwa mahakamani hapo akikabiliwa na kosa
la kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa X, akidaiwa kutenda kosa hilo
chini ya kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015
akidaiwa kutenda kosa hilo Januari 9, 2025.
0 Maoni