Wananchi wilayani Nyasa mkoani Ruvuma, wameipongeza
Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa
kuboresha miundombinu na kujenga barabara za mitaa katika mji mdogo wa
Mbambabay kwa kiwango cha lami.
Wamesema, ujenzi wa barabara hizo umesaidia kurahisisha
huduma ya usafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine, kuondoa adha ya vumbi
kipindi cha kiangazi na matope kila inapofika msimu wa mvua pamoja na maeneo yao
kupanda thamani ikilinganishwa na siku za nyuma.
Petro Zambala mkazi wa Mbambabay alisema, uamuzi wa
Serikali kujenga barabara kwa kiwango cha lami katika mji huo utaharakisha
maendeleo na kuchochea kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na wilaya ya Nyasa.
“Ni jambo la faraja kwetu kujengewa barabara za lami
kwenye mitaa yetu, kukamilika kwa barabara hii kumesaidia kupunguza gharama za
maisha na usafiri.”
Bw. Nikaya Mbalale mkazi wa Mbambabay alisema, tangu
Serikali ya awamu ya Sita ilipoingia madarakani kuna mabadiliko makubwa katika
mji huo hasa baada ya TARURA kupatiwa fedha nyingi ambazo zimewezesha kuboresha
miundombinu ya barabara za lami, tofauti na siku za nyuma ambapo barabara
nyingi za mitaa zilikuwa za vumbi.
Alisema, kuimarisha na kuboreshwa kwa barabara hizo
zimehamasisha na kuwavutia watu wengi kwenda kuwekeza katika Mji wa Mbambabay ambao
wananchi wake wanategemea shughuli za uvuvi na kilimo ili kuendesha maisha yao.
Alisema, Serikali imemaliza kero hiyo, sasa magari
yanafika na kuondoka kwenye mji wa Mbambabay muda wowote na wananchi wanafanya
shughuli zao za uzalishaji mali.
Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Nyasa, Mhandisi Derick
Theonest alisema, TARURA inaendelea kufanya jitihada mbalimbali kwa kujenga
barabara za lami ili kuboresha mazingira na maisha ya wananchi wa mji wa utalii
wa Mbambabay na wilaya ya Nyasa kwa ujumla.
Alisema, hadi sasa wamebakisha kilometa1 ili kukamilisha
barabara za lami katika mji wote wa Mbambabay na kuishukuru Serikali kwa
kuendelea kuipatia TARURA fedha kwa kujenga miundombinu ikiwemo barabara za
lami ambazo zina mchango mkubwa katika kuchochea na kuharakisha maendeleo.
Amewataka wananchi kuhakikisha wanatunza na kulinda
miundombinu ya barabara hizo ili ziweze kudumu kwa muda mrefu kwani zinatumia
fedha nyingi kuzijenga.

0 Maoni