Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amebainisha kuwa
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imenunua tani 2.6 za dhahabu inayochimbwa na
kusafishwa hapa nchini ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na changamoto
ya upungufu wa fedha za kigeni, kuboresha akiba ya fedha za kigeni, na
kuimarisha thamani ya shilingi ya Tanzania.
Amesema hayo leo Januari 22, 2024, jijini Dodoma, wakati
akiwasilisha taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini,
taarifa inayohusu utendaji wa viwanda vya kusafisha dhahabu nchini kwa kipindi
cha Machi hadi Desemba 2024 pamoja na mwenendo wa ununuzi wa dhahabu
unaotekelezwa na BoT.
Mwenendo wa Ununuzi wa Dhahabu BoT
Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, tarehe 1 Oktoba 2024, Tume
ya Madini ilitoa tangazo linalowataka wachimbaji na wafanyabiashara wa dhahabu
kutekeleza takwa la Kifungu cha 59 cha Sheria ya Madini Sura 123, ambalo
linawataka kutenga asilimia 20 ya dhahabu na kuiuzia BoT kupitia viwanda vya
usafishaji vilivyoidhinishwa.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, Tangu kutolewa kwa tangazo hilo
hadi Januari 21, 2025, BoT imefanikiwa kununua tani 2.6 za dhahabu kutoka kwa
wachimbaji wa kati, wachimbaji wadogo, na wafanyabiashara wa dhahabu. Thamani
ya dhahabu hiyo ni zaidi ya shilingi bilioni 570 kwa mujibu wa bei ya soko la
dunia ya tarehe 22 Januari 2025” amesema Mhe. Mavunde.
Halikadhalika, Waziri Mavunde amesisitiza kuwa, kupitia
mpango huo wa BoT, lengo la Serikali ni kuifanya Tanzania kuwa moja ya mataifa
10 yenye hifadhi kubwa ya dhahabu barani Afrika kwa ustawi wa taifa.
Ongezeko la Mapato ya Serikali
Kwa upande wa mapato, Waziri Mavunde amebainisha kuwa,
mwenendo wa ukusanyaji wa mrabaha kwa upande wa madini ya dhahabu umeendelea
kuimarika na kwamba kuanzia Julai 1, 2024 hadi Desemba 31, 2024, Serikali
iliingiza shilingi bilioni 400.22 kutokana na mauzo ya kilogramu 34,826.75 za
dhahabu, ikiwa ni ongezeko la asilimia 5.55 ikilinganishwa na kipindi kama
hicho mwaka 2023, ambapo kilogramu 32,995.54 ziliuzwa na Serikali kupata
shilingi bilioni 278.86.
Maendeleo ya Kiwanda cha Kusafisha Makinikia – Kahama
Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde aligusia maendeleo
ya Kiwanda cha Kusafisha Makinikia cha Tembo Nickel Refining Limited,
kitakachojengwa Kahama, mkoani Shinyanga katika eneo ambalo awali lilikuwa
likitumiwa na Mgodi wa Buzwagi, ambao umesitisha shughuli za uzalishaji wa
dhahabu.
Amefafanua kuwa mradi wa Kiwanda hicho ni moja ya miradi
machache barani Afrika inayozalisha bidhaa iliyotayari kwa matumizi, hivyo
unatarajiwa kuleta tija kubwa kwa uchumi wa nchi, sambamba na kuimarisha
Mchango wa Sekta ya Madini.
Faida za Mpango wa BoT
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na
Madini, Dkt. Mathayo David, amepongeza juhudi hizo na kueleza kuwa hatua hiyo
itasaidia kuimarisha shilingi ya Tanzania, kuimarisha akiba ya dhahabu, na
kuiweka nchi katika orodha ya mataifa yenye hifadhi kubwa ya dhahabu
ulimwenguni.
Juhudi hizo ni sehemu ya mikakati ya Serikali kupitia
Wizara ya Madini kuhakikisha kuwa Sekta ya Madini inatoa mchango mkubwa zaidi
kwa uchumi wa Taifa na ustawi wa wananchi.



0 Maoni