Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emanuel Tutuba
amesema kuwa noti mpya za Tanzania zenye Saini ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwingulu Nchemba (Mb) na yeye mwenyewe, za toleo la mwaka 2010, zitaingia kwenye
mzunguko kuanzia Februari MOSI mwaka huu.
Gavana Tutuba amesema hayo Jijini Dar es Salaam wakati
akimkabidhi Mhe. Dkt. Nchemba, noti kifani za Shilingi elfu kumi, elfu tano, elfu mbili na Shilingi elfu moja, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, kwa
mujibu wa Sheria na Taratibu zinazosimamia masuala ya fedha nchini.
“Mheshimiwa Waziri, ninayofuraha kukujulisha kuwa zoezi
letu la uchapaji upya wa Noti kwa marejeo ya toleo la mwaka 2010, limekamilika
na tayari tumewajulisha wananchi kupitia taarifa niliyoitoa kupitia Gazeti la
Serikali,” alisema Bw. Tutuba.
Gavana Tutuba alifafanua kuwa noti hizo zitatumika
sambamba na Noti zilizopo hivi sasa, zinamwonekano wa Noti zinazotumika hivi
sasa zilizotolewa Mwaka 2010, ikiwemo alama za usalama, ukubwa, rangi na mambo
mengine, isipokuwa ina marekebisho kwenye saini ya Waziri wa Fedha, na Gavana
wa Benki Kuu ya Tanzania.
“Saini ya aliyekuwa Waziri wa Fedha ambaye hivi sasa ni
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor
Mpango imebadilishwa na kuwekwa Saini yako Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na
Saini ya aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania aliyestaafu, Prof. Florens
Luoga, imebadilishwa na kuwekwa Saini ya Gavana wa Benki Kuu wa sasa, Bw.
Emmanuel Tutuba,” aliongeza Bw. Tutuba.
Akizungumza baada ya kupokea sampuli za noti hizo mpya,
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alimshukuru Mhe. Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu jambo hilo kufanyika na kumpongeza Gavana wa
Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, kwa kusimamia mchakato wa uchapaji
wa noti hizo kwa weledi na uadilifu mkubwa.
“Mpaka kufikia hatua hii ni heshima kubwa kwa Taifa letu
na inaendeleza heshima ya wataalam wetu mnavyoweza kusimamia kwa umakini mambo
yenye maslahi mapana kwa nchi yetu,” alisema Dkt. Nchemba. 
Mhe. Dkt. Nchemba ameridhia noti hizo ziingizwe kwenye
mzunguko na kuanza kutumika kama ilivyopangwa Februari mosi mwaka huu.

 
 
 
 
 
 
 
 
0 Maoni