SERIKALI
kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) inajipanga kufungua
mawasiliano kwa kuunganisha Barabara ya Langa-Mkuu na Msitu wa Tembo katika
Kata ya Msitu wa Tembo- Ngorika kuelekea Ngange wilayani Simanjiro, Mkoa wa
Manyara.
Kaimu
Meneja wa Tarura Wilaya ya Simanjiro, Mhandisi Naftari Chaula amesema hayo
wakati wa ukaguzi wa utekelezaji wa ujenzi na matengenezo ya barabara wilayani
humo.
Mhandisi
Chaula amesema Barabara hiyo imekuwa ikikumbwa na mafuriko pamoja na sehemu
nyingine kutofunguliwa kutokana na kuwa na makorongo mengi yaliyosababishwa na
mvua nyingi.
Amesema
kwa mwaka huu wa fedha wanatarajia kukamilisha ujenzi wa madaraja kwa zaidi ya
asilimia 70 na tayari mkandarasi yupo eneo la ujenzi akiendelea na uchimbaji na
upangaji wa mawe na kwamba kukamilika kwa ujenzi huo kutafungua mawasiliano
kati ya Kata ya Ngorika na Msitu wa Tembo na kuwezesha usafirishaji wa mazao ya
uvuvi kutoka Bwawa la Nyumba ya Mungu.
“Wananchi
wamekuwa wakipata shida sana katika shughuli za usafirishaji wa mazao ya uvuvi,
bidhaa nyingine za kilimo na hata wananchi wa Ngorika kwenda Hospitali ya Kata
ya Msitu wa Tembo na Hospitali ya KCMC mkoani Kilimanjaro na mahali kwingine
kwaajili ya matibabu,” alisema Mhandisi Chaula.
Kwa
upande wao wananchi wa Kata hiyo wameishukuru Serikuli kupitia Wakala hiyo kwa
kuwapelekea mradi huo ambao wanasema utasaidia kuondoa changamoto walizokuwa
wakikutana nazo.
Thomas
Sokoine Mkazi wa Kijiji cha Londoto Kata ya Msitu wa Tembo amesema kujengwa kwa
daraja katika korongo hilo kutasaidia wananchi wakiwemo watoto kutokukwama tena
kuvuka upande wa pili.
Kwa
upande wake Robert Juma dereva wa lori la mizigo amesema barabara hiyo imekuwa
ni changamoto sana hususani wakati wa mvua na kumshukuru Rais Samia kwa
kuwapelekea mradi huo wa ujenzi wa makalavati akisema anaamini utawaondolea
changamoto wanayokumbana nayo ikiwemo kusitisha shughuli za usafirishaji hasa
katika kipindi cha mvua.
Naye
Jorum Yohana Mkazi wa Msitu wa Tembo amesema maeneo yao yalikuwa ni hatarishi
sana kutokana na maji kuleta adha kubwa kwa wananchi na kuishukuru Serikali kwa
kuwawekea lami kipande cha Kilometa 1 na kuongeza kuwa serikali imeongeza fedha
kwa kuwajengea makalavati, hivyo wanaamini barabara hiyo ikikamilika
itawasaidia katika shughuli za kilimo, ufugaji na biashara zitaendelea kuinuka
na hivyo kupata unafuu wa kimaisha na kuweza kuwainganisha kati ya Mkoa wa
Manyara na Kilimanjaro.
0 Maoni