Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Mauritania, Mheshimiwa
Mohamed Ould Ghazouani, amewasili jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kushiriki
Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati.
Alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius
Nyerere, Mheshimiwa Mohamed Ould Ghazouani, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja
wa Afrika, alipokelewa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Festo Dugange,Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam
Mheshimiwa Albert Chalamila pamoja na viongozi wengine wa Serikali.
Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati unafanyika
jijini Dar es Salaam tarehe 27 na 28 Januari 2025 katika Kituo cha Kimataifa
cha Mikutano cha Julius Nyerere.
Mkutano huo unawaleta pamoja Wakuu wa Nchi za Afrika, wataalam wa nishati, viongozi wa sekta binafsi, na washirika wa maendeleo kwa ajili ya kujadili mikakati ya kukabiliana na changamoto za nishati na kuchangamkia fursa za bara hili. Kipengele muhimu cha mkutano huu kitakuwa kupitishwa kwa Azimio la Dar es Salaam, linalosisitiza dhamira ya pamoja ya viongozi wa Afrika kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika, nafuu, na endelevu kwa maendeleo ya bara la Afrika.




0 Maoni