Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan
amesikitishwa na Kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Liwale Ndugu.
Kindamba Milingo.
Akiwasilisha salamu za Chama cha Mapinduzi
kwa waombolezaji waliojitokeza katika Msiba huo Uliofanyika jana Januari 08,
2025, Nyumbani kwa Marehemu Pulipwite Liwale Mjini mkoani Lindi, Mjumbe wa
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
amesema Rais anatambua mchango mkubwa uliofanywa na marehemu enzi ya uhai wake
katika kukijenga Chama cha Mapinduzi.
"Kwa niaba ya Mwenyekiti wetu wa Chama,
Katibu Mkuu na viongozi wengine naomba kuwasilisha salamu za rambirambi kutoka
Chama cha Mapinduzi CCM, viongozi wetu hawa wote wameguswa na kifo cha Milingo
na wanatambua kazi kubwa aliyoifanya katika kukijenga chama kwenye ngazi ya
Wilaya alipokuwa anahudumu.”
Amesema marehemu mzee Milingo alikuwa
kiunganishi kikubwa kati ya Chama na Serikali katika kuhakikisha wanafuatilia
utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ili kusaidia kuongeza kasi ya
maendeleo ndani ya Wilaya ya Liwale.
Mheshimiwa Majaliwa amesema ni vyema
wanachama wa CCM wakaendelea kuenzi mazuri yote yaliyofanywa na Mwenyekiti huyo
pamoja na kuendelea kumuombea.
"Mzee wetu amefanya kazi kubwa ndani ya
chama, yeye pamoja na viongozi wengine walikiunganisha Chama na Mkoa wa Lindi.”
Naye Mbunge wa Liwale Zuberi Kuchauka amesema
Wilaya ya Liwale imepoteza kiongozi Mahiri na Mwanachama Mtiifu wa Chama cha
Mapinduzi ambaye alijitoa kwa nguvu zote
kukijenga chama hicho.
Marehemu Mzee Milingo alifariki tarehe 6
Januari 2025 katika hospitali ya Rufaa ya Sokoine Mkoani Lindi, amezikwa katika
makaburi ya Nanganda Liwale Mkoani Lindi.
0 Maoni