Katika kutekeleza upatikanaji wa Bima ya Afya
kwa Wote, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) unaingia makubaliano na mawakala
nchini ili kufanikisha usajili wa wananchi wengi zaidi katika huduma ya bima ya
afya.
Hayo yamebainishwa jana Januari 8, 2025,
kwenye kikao kazi kati ya NHIF, Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA) na Mawakala
nchini.
Usajili kwa njia ya mawakala unatarajiwa kuanza
Februari mwaka huu ambao wataweza kuwafikia wananchi katika maeneo yote na
kuwasajili na bima ya afya.
Akizungumzia kuanza kwa usajili huo,
Mkurugenzi Mkuu Dkt. Irene Isaka amesema kuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha
wananchi wote wanakuwa ndani ya Mfumo wa Bima ya Afya hivyo Mawakala watasaidia
kufikia malengo hayo.
"NHIF tumeona umuhimu wa kufanyakazi kwa
kushirikisha mawakala ili wananchi waweze kufikiwa walipo na kusajiliwa kwenye
bima ya afya ili waweze kupata huduma za matibabu bila kikwazo cha fedha. Kwa
kaya zisizo na uwezo, Serikali imeweka mazingira wezeshi ili nao wapate Bima ya
Afya. Nawaomba sana tuunge mkono juhudi za Serikali chini ya uongozi mahiri wa
Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa na Bima ya Afya kwa wote,” alisema Dkt.
Isaka.
Kwa upande wa mawakala hao, kwa pamoja
wameupongeza mfuko kwa hatua ya kuwashirikisha katika eneo la kuwafikia
wananchi lakini pia maboresho makubwa ambayo yamefanyika katika mifumo yake na
vifurushi vipya ambavyo vina huduma nyingi ikilinganishwa na awali.
NHIF inaendelea kukutana na makundi
mbalimbali kwa ajili ya uelimishaji wa utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote
lakini pia kuweka mikakati ya kuwahudumia wananchi kwa kuwafikia na kuwasajili.
0 Maoni