Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.
Dunstan Kitandula (Mb) amemtaka mkandarasi Kampuni ya China Henan International
Cooperation Group (CHICO) kutoka China inayojenga uwanja wa ndege wa Mtemere
uliopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Nyerere kukamilisha ujenzi kwa mujibu wa
mkataba iliyowekeana na serikali.
Naibu Waziri ameyasema hayo wakati wa ziara
ya kukagua Miradi ya Maendeleo inayojengwa na Mradi wa kuboresha usimamizi wa
maliasili na kukuza utalii kusini mwa Tanzania(REGROW) katika hifadhi ya Taifa
Nyerere.
Mhe. Kitandula aliwataka watumishi
wanaosimamia miradi hiyo kuhakikisha kuwa miradi hiyo inakamilishwa kwa wakati
na thamani ya fedha iliyotumika kujenga miradi hiyo inaonekana katika ubora wa
miradi hiyo.
Aidha, zaidi ya bilioni 40 zimetumika kufadhili
miradi mbalimbali ya ujenzi katika hifadhi ya Taifa Nyerere ikiwemo ujenzi wa
Uwanja wa Ndege, Kujenga makazi ya Askari ndani ya Hifadhi, kujenga sehemu za
kulaza wageni, kujenga Lango la Kuingilia hifadhini pamoja na ununuzi wa
mitambo ya kutengenezea barabara na magari kwa ajili ya shughuli za utawala.
Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na
Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) pamoja na ujenzi wa miundo mbinu
mbalimbali ndani ya hifadhi hiyo, mradi umekuwa ukishiriki katika kukabiliana na migogoro baina ya binadamu na
wanyamapori kwa kuwezesha mafunzo kwa VGS 150 kutoka katika vijiji 15 pembezoni
mwa Hifadhi ya Taifa Nyerere.
"Kupitia uboreshaji huu wa miundombinu
naiona hifadhi hii kuwa chachu ya kuongeza idadi kubwa ya watalii nchini lakini
pia itapelekea kuchangia fedha za kigeni kwa wingi katika kapu la Taifa."
Aliongeza Mhe. Kitandula.
Aidha, Mheshimiwa Kitandula ameutaka uongozi
wa Hifadhi ya Taifa Nyerere kushirikiana na viongozi wa vijiji ambavyo
vinapakana na hifadhi hiyo hasa pale ambapo kunakuwa na changamoto ya wanyama
wakali na waharibifu.
Na. Anangisye Mwateba- Hifadhi ya Taifa
Nyerere
0 Maoni