Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
na Msemaji Mkuu wa Serikari Ndg. Gerson Msigwa akagua na kuridhishwa na
utekelezaji wa Mradi wa ujenzi wa kiwanja cha ndege Kikoboga, Mradi
unaotekelezwa kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Kuboresha
Usimamizi wa Maliasili na kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW).
Akiwa katika uwanja huo, Ndg. Gerson Msigwa alishuhudia
ndege zaidi ya tano za mashirika tofauti zilizokuwa zimeshusha na kusubiria
watalii kutoka mataifa mbalimbali.
Hata hivyo, Msemaji Mkuu huyo alisema, “Serikali
imejidhatiti kuboresha viwanja vingi vya ndege katika Hifadhi za Taifa Tanzania
ili kuwarahishia watalii wetu kufika hifadhini kwa wakati na kupata ile thamani
ya fedha wanazotoa.”
Aidha aliongeza, “Leo tumekiona kiwanja hiki kimoja lakini
serikali kupitia mradi wa “REGROW” pia, inaendelea kukamilisha viwanja vingine
vya ndege vyenye hadhi na ukubwa wa aina hii katika Hifadhi za Taifa Ruaha na
Nyerere. Hivyo kukamilika kwa viwanja hivi na miundombinu mingine ya kisasa
katika medani ya utalii itaongeza kasi ya ukusanyaji wa maduhuli na kasi ya
ukuaji wa sekta hii nyeti kwa faida ya taifa letu.”
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi - Augustino Massesa
ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mikumi alisema, “Ndege nyingi tunazozipokea
katika hifadhi hii hutokea Zanzibar na zimeendelea kuleta matokeo chanya na
tunatarajia siku za usoni tutakuwa na watalii wengi mithili ya wale
wanaotembelea Serengeti.”
Akitoa Maelezo ya Kiwanja hicho kwa Msemaji Mkuu wa
Serikali, Afisa Uhifadhi Mwandamizi Herman Baltazari alisema kuwa Uwanja huo ni
wa kisasa na umekidhi vigezo vinavyokubalika na Mamlaka ya Viwanja vya ndege
kwani una urefu wa kilometa 2.4 kwenye njia ya miruko, kuna jengo la abiria
lenye uwezo wa kutosheleza abiria 140 kwa wakati mmoja, majengo ya zimamoto na
nishati itakayotumika katika uwanja huo sambamba na eneo la kuegesha magari
yatakayokuja kupokea au kuleta wageni wanaoondoka.
Mbali na kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii ndani ya
hifadhi hiyo huku shauku kubwa aliyokuwa nayo ni kumuona Kasongo (Ngiri), pia
Ndg. Msigwa alikagua mradi wa ujenzi wa “Cottages” pamoja na Uwanja wa mpira wa
miguu uliopo ndani ya hifadhi hiyo.
Wakati akiukagua uwanja huo wa mpira wa miguu, Msemaji huyo
alisema kuwa Serikali itashirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa
uangalizi wa TANAPA kuhakikisha uwanja huo unaboreshwa ili kukidhi viwango
vinavyokubalika na TFF na CAF ili timu kubwa zinazoshiriki mashindano ya
kitaifa na kimataifa waweze kuutumia.
Mkutano huo wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Ndg. Gerson Msigwa umefanyika leo Januari 25, 2025 ndani ya Hifadhi ya Taifa Mikumi, huku waandishi wa Habari wakishuhudia makundi mbalimbali ya watalii huku pembeni wakifurahia kuona wanyamapori.
Na. Jacob Kasiri - Mikumi
0 Maoni