WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wasimamizi wa miradi inayotekelezwa na Serikali ikiwemo ya elimu kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaolingana na thamani ya fedha iliyotolewa.
Ametoa
wito huo leo (Jumatatu Januari 06, 2025) wakati wa ufunguzi wa Skuli ya
Sekondari ya Makoba iliyopo Mkoa wa Kaskazini Unguja, Zanzibar. Ufunguzi wa
skuli hiyo ni sehemu ya shamrashamra kuelekea maadhimisho ya miaka 61 ya
Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Amesema
kuwa Serikali imeendelea kutenga rasilimali fedha kwa ajili ya maendeleo ya
sekta ya elimu ambayo kwa kiasi kikubwa imewezesha kuweka mazingira bora ya
upatikanaji wa elimu ikiwemo ujenzi wa miundombinu.
Aidha,
Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema kuwa katika kipindi cha miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu
ya Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein
Ali Mwinyi ameendelea kuipa hadhi sekta ya elimu kwa kuhakikisha kunakuwa na
ufanisi wa utoaji wa huduma za elimu.
“Sina
shaka leo hii chini ya Jemedari Dkt. Hussein Ali Mwinyi sote tunashuhudia
mwendelezo wa hatua kubwa ya kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu nchini.
Suala hili ni la kujivunia kwa kuwa ni Matunda ya Mapinduzi ambayo sasa
yanafikisha miaka 61 tangu kuasisiwa kwake.”
Kadhalika,
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein
Mwinyi, imeendelea kufanya mageuzi makubwa ya elimu katika kuhakikisha kunakuwa
na ufanisi wa utoaji wa huduma za elimu nchini. “Mageuzi hayo ni pamoja na
kutekeleza mtaala mpya wa umahiri utakaomwezesha mtoto kujifunza kwa vitendo na
kumudu kasi kubwa ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia.”
Ameongeza
kuwa Serikali imeendelea kutekeleza mipango, mikakati na kufanya jitihada za
makusudi za kuhakikisha kunakuwa na maendeleo kwenye sekta zote za kijamii ili
kuleta tija inayotarajiwa kwa wananchi bila ubaguzi wa aina yoyote.
Kwa
upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Lela Mohamed Mussa amesema
kuwa Rais Dkt. Mwinyi ameendeleza ari ya Waasisi wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar katika kuhakikisha analeta mageuzi makubwa katika Sekta ya Elimu.
“Serikali
hii iliahidi kuboresha miundombinu ya madarasa kwa shule za msingi kwa kujenga
madarasa 1,000 na 500 kwa ngazi ya Sekondari na mpaka sasa kwa ngazi ya msingi
imejenga madarasa 2,893 na ngazi ya Sekondari imejenga madarasa 1,917.”
Ujenzi
wa Shule hiyo ambao umefikia asilimia 100 umegharimu kiasi cha shilingi bilioni
6.1 ambazo zimetolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais
Dkt Hussein Ali Mwinyi.
0 Maoni