Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amefanya ziara katika Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma kukagua maendeleo ya ujenzi majengo ya Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu pamoja na Wizara ya Nishati ambayo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 88.
Akizungumza
baada ya kukagua na kupata maelezo ya wataalam na wasimamizi wa majengo hayo,
Naibu Waziri Mkuu Biteko amewapongeza wakandarasi kwa hatua iliyofikiwa na
kuagiza majengo yakamilishwe kabla ya mwezi Aprili, 2025.
“Serikali
chini ya Rais Samia imefanya kazi kubwa, tayari imetoa zaidi ya asilimia 90 ya
malipo kwa wakandarasi kwa maana ya kwamba ni kiasi kikubwa zaidi ya ukamilifu
wa jengo, Najua SUMA JKT mkifanya kazi kwa operesheni mnaweza kukamilisha
ujenzi wa jengo hili hata kabla ya muda uliopangwa,” amesema Dkt. Biteko.
Msimamizi
wa Ujenzi Jengo la Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, kutoka SUMA JKT
Kanali Mbaraka Magogo ameomba Serikali iwaongezee muda wa miezi mitatu kuanzia
sasa ili kukamilisha ujenzi na majengo yatumike ifikapo mwezi Aprili, 2025.
Katika
hatua nyingine, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko
ametembelea jengo la Wizara ya Nishati ambapo amemtaka mkandarasi ambaye ni
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuharakisha ukamilishaji ujenzi wa jengo hilo
na lianze kutumika kabla ya mwezi Aprili, mmwaka huu.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu,
Mhe. Ummy Nderiananga amemshukuru Naibu Waziri Mkuu kwa maelekezo yake na
kusema Ofisi itaendelea kusimamia kwa karibu ili kuhakikisha kwamba malengo
yanafikiwa kama ilivyopangwa.
“Kwa
niaba ya Waziri Nchi Mhe. Lukuvi (William Lukuvi) namshukuru Mheshimiwa Naibu
Waziri Mkuu kwa ziara hii ambayo ni chagizo kwetu kuhakikisha kwamba ujenzi wa
majengo haya unakamilika kwa wakati kama walivyoomba wakandarasi, kwa kuwa sisi
ni waratibu inabidi tuwe mfano kwa wengine,” amesema Mhe. Ummy.
Naye
Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felichesmi Mramba amemhakikishia Naibu
Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kuwa fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi
wa Wizara hiyo ziko katika hatua nzuri na amekuwa akiwasiliana na HAZINA kwa
ajili ya upatikanaji wake.
“Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, tuko katika hatua nzuri hata leo asubuhi nimezungumza na PST (Katibu Mkuu Wizara ya Fedha) na nimehakikishiwa kwamba fedha hizo zitapatikana,” amesema Katibu Mkuu Mramba.
Na
Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
0 Maoni