Lema amtaka Mbowe amuachie uenyekiti Tundu Lissu

 

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini Godbless Lema amemtaka Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Bw. Freeman Mbowe aache kuwania nafasi hiyo na badala yake apumzike na kumuachia Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara Tundu Lissu awe mwenyekiti wa chama hicho.

Lema ametoa kauli hiyo leo Jijini Dar es Salaam, wakati akiongea na waandishi wa habari, ambapo amesema Mbowe amekuwa kwenye chama kwa muda wa miaka 30, na amekiongoza CHADEMA kwa muda wa miaka 21, inatosha sasa anapaswa kumuachia mtu mungine akiongoze chama.

“Mwenyekiti ni ndugu yangu, ni kaka yangu tunatoka wote Machame lakini leo hapa nimekuja kutangaza kwamba katika uchaguzi huu unaofanyika keshokutwa nafanya uamuzi mgumu sana Mbowe ni Kaka yangu lakini leo nimekuja kumuomba apumzike amuachie Lissu afanye kazi ya uenyekiti, Mbowe apumzike apumzike,” alisema Lema.

“Na tunaposema apumzike hatumaanishi hana nguvu, inawezekana uwezo wake wa kuongoza umefika mwisho bila yeye kujua, kuna wakati kwenye hizi kazi unaona mivuragano hata mimi niliiona pale Arusha hata kama mingine inachangiwa na watu wa nje lakini niliona nikasema nikilazimisha kugombea ili nishinde itabidi nifungie watu kwenye maghala, nikatangaza sitogombea uenyekiti wa Kanda,” aliongeza kusema Lema.

Ukaja uchaguzi wa kanda niliona pia minyukano sikugombea, sasa nimekuja kumwambia mwenyekiti haya majibizano mitandaoni na minyukano, nafahamu Katiba inamruhusu kuendelea lakini kwa sasa watu wamepatikana wanataka nafasi yake na huwezi kumtilia mashaka Lissu ambaye amekuwa Makamu Mwenyekiti, Mnadhimu Mkuu wa Chama, Mwanasheria Mkuu wa chama, usipomuamini makamu wako kumuachia chama unataka kumuachia nani ?, alihoji Lema.

Chapisha Maoni

0 Maoni