Kazi kubwa ya kutangaza vivutio vya utalii vya nchi yetu
duniani iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan inaendelea kudhihirika na kishindo chake kutikisa katika Hifadhi
ya Urithi wa Utamaduni wa Dunia ya Magofu ya Kale ya Kilwa Kisiwani na Songo
Mnara ambayo inaendelea kupokea makundi ya watalii wa nje kutoka Mataifa
mbalimbali.
Hifadhi hiyo iliyo chini ya usimamizi wa Mamlaka ya
Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA imefungua ukurasa mpya wa mwaka 2025
Kwa kupokea watalii wa kigeni kutoka Mataifa mbalimbali ambapo Januari 18, 2025
ilipokea wageni 98 na jana Januari 22, 2025 imepokea Kundi lingine la watalii
wapatao 173 kutoka Mataifa ya Uingereza,
Finland, Sychelles, Marekani, Sweden, Australia na Ireland ambao Kwa kutumia
meli kubwa aina ya Hebridean Sky walifika hifadhini humo Kwa lengo la kutalii.
Hatua iliyochukuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kucheza filamu ya Royal Tour iliyokuwa
na lengo la kuhuisha Sekta ya Utalii nchini iliyokuwa imefifishwa na janga la
UVIKO 19, janga linalotajwa kusababisha mdororo wa uchumi duniani imesaidia
kuchechemua Sekta ya utalii nchini na kuifanya TAWA kuwa mojawapo ya taasisi za
kiuhifadhi zilizonufaika Kwa kupata Idadi kubwa ya wageni wanaotembelea katika
maeneo inayosimamia kwa shughuli za utalii wa picha na uwindaji wa kitalii.
Ikumbukwe kuwa katika kipindi cha Mwaka 2023/24 TAWA
kupitia Hifadhi ya Urithi wa Utamaduni wa Dunia Magofu ya Kilwa Kisiwani na
Songo Mnara iliweza kupokea meli 9 za kitalii na jumla ya watalii wa Kigeni
1,047.
Na. Beatus Maganja- Kilwa




0 Maoni