Mahakama ya Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza imemhukumu kifungo cha miezi sita jela Rajabu Reli (22), mkazi wa Sengerema baada ya kukutwa na hatia ya kuvaa sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) bila ruhusa.
Hukumu hiyo imetolewa jana Januari 07, 2025
katika shauri la jinai namba 445 la mwaka 2025 na Hakimu Mfawidhi wa mahakama
hiyo Mhe. Evodius Kisoka mbele ya mwendesha mashtaka wa Serikali Nyamhanga
Tissoro.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyosomwa na
mwendesha mashtaka wa Serikali Nyamhanga Tissoro mbele ya hakimu Evodius
Kisoka, mshtakiwa alitenda kosa hilo mnamo tarehe 05.12.2024 huko kijiji cha
Kasisa, Wilaya ya Sengerema kinyume na kifungu cha 178(1) cha sheria ya kanuni ya
Adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.
Mshtakiwa alifikishwa mahakamani Januari
07.2025 na kusomewa shitaka la kuvaa sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania bila
ruhusa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Baada ya kusikiliza pande zote za ushahidi
hakimu Evodius Kisoka alijiridhisha kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa
Jamhuri ni mzito na haukuacha shaka lolote.
Hata hivyo, mshtakiwa alipopewa nafasi ya
kujitetetea kwa nini asipewe adhabu; aliomba Mahakama hiyo imuachie huru kwa
kuwa ni mkosaji wa mara ya kwanza na alivaa ili akubaliwe na mchumba wake.
"Mhe. Hakimu naomba nisamehewe kwa kuwa
ni kosa la kwanza na nilivaa na kwenda kumuonesha mchumba wangu kuwa mimi ni
Askari ili asinikatae," alisema Rajabu akiomba huruma ya Hakimu.
Ombi hilo lilitupiliwa mbali na Hakimu Kisoka
na kutoa adhabu hiyo ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama ya
Rajabu.
0 Maoni