Tanzania, itapokea kiasi cha Yen za Japan bilioni 22.742 sawa na shilingi bilioni 354.45 kama mkopo nafuu, kutoka serikali ya Japan kufuatia kusainiwa kwa mikataba miwili, baina ya Wizara ya Fedha kwa upande wa Tanzania na Ubalozi wa Japan na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA).

Mikataba hiyo miwili imesainiwa jijini Dar es Salaam, leo Januari 14, 2025, ambapo Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alitia saini kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Balozi wa Japan nchini, Mhe. Yasushi Misawa, kwaniaba ya Serikali ya Japan, na Makamu wa rais wa JICA, Bi. Katsura Miyazaki.

Akizunguzma katika hafla hiyo iliyoshuhudiwa na Naibu Waziri wa Mamabo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi, Naibu Waziri wa Mamabo ya Nje wa Japan, Mhe. Fujii Hisayuki, Balozi wa Tanzania nchini Japan, Mhe. Baraka Luvanda, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Jennifer Omolo na Mtendaji Mkuu wa Benki ya Maendeleo, (TADB), Bw. Frank Nyabundege, Mhe. Nchemba alisema, fedha hizo ni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa uendelezaji wa kilimo vijijini.

Alisema ufadhili huo utasimamiwa na JICA kwa niaba ya serikali ya Japan, na kwa upande wa Serikali ya Tanzania mradi utatekekezwa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB).

 “Utekelezaji wa mradi huu utachochea ukuaji wa sekta ya kilimo kwa kuongeza uzalishaji kwa wakulima kupitia mikopo nafuu ya muda wa kati na muda mrefu kwa wakulima, ili kuwekeza katika kilimo cha kisasa,” alisema Dkt. Nchemba.