Vyuo na taasisi zinazotoa elimu ngazi ya Kati ikiwemo
Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), zimetakiwa kuboresha mitaala yake ya masomo
ili iendane na mahitaji ya sasa ya soko la ajira kimataifa sambamba na mahitaji
ya kijamii na kiuchumi.
Hayo yamebainishwa leo Januari 21, 2025 na Naibu Waziri
Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko katika Maadhimisho ya miaka 60
ya chuo hicho kilichoanzishwa Januari 21, 1965 jijini Dar es Salaam.
"Serikali inasisitiza matumizi ya teknolojia za
kisasa na mbinu za kujifunza zinazojibu changamoto za kimataifa, " amesema
Dkt. Biteko.
Amesema kuwa Serikali inazitaka taasisi za elimu ya kati
kikiwemo Chuo cha CBE kuweka mkazo kwenye mafunzo ya ujasiriamali, ili wahitimu
wake waweze kuchangia kikamilifu katika uchumi wa taifa kupitia biashara bunifu
na ajira binafsi.
Aidha, taasisi za elimu, zikiwemo vyuo kama CBE,
amezitaka kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi ili kuhakikisha mafunzo
yanayotolewa yanakidhi mahitaji ya soko la ajira na pia kusaidia kukuza sekta
hiyo kwa utafiti na mafunzo.
Ameongeza kuwa, Serikali inahimiza vyuo vya elimu ya
biashara kufanya tafiti za kina zinazosaidia kutatua changamoto za kiuchumi,
kuimarisha sera za biashara, na kubuni suluhisho endelevu.
"Serikali imeelekeza taasisi kama CBE zihakikishe
kwamba fursa za elimu zinafikia makundi yote ya jamii, wakiwemo wanawake,
vijana, na watu wenye ulemavu, ili kuongeza ushiriki wa makundi yote katika
uchumi wa taifa, " ameongeza Dkt. Biteko.
Naye, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Selemani Jafo
amesema CBE ni kitovu cha biashara
nchini na kimeweza kujenga mahusiano na nchi mbalimbali kimataifa ikiwemo nchi
ya China na Ujerumani na ni ufunguo wa ufanyaji wa biashara katika kampasi zote
nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu
Nchemba amesema CBE imekuwa ikifanya kazi nzuri na kina mchango mkubwa katika
ukuaji wa sekta ya fedha hapa nchini.
“Fedha na Biashara na Uwekezaji havitengamani lakini
mafanikio yote yaliyofikiwa lazima tumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono na uongozi wake
uliotuheshimisha, " amesema Mhe. Nchemba.
Vile vile, Mkuu wa Chuo cha CBE, Prof. Edda Lwoga amesema
kuwa katika maadhimisho ya miaka 60 ya CBE wemekuwa wakitoa elimu ya biashara
kwa makundi mbalimbali ya kijamii na pia wametoa mafunzo ya muda mfupi kwa
wadau mbalimbali wa biashara.
0 Maoni