Jeshi la Polisi mkoani Pwani linamshikilia mtuhumiwa
mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa kwa tuhuma za kukutwa na picha mjongeo za
utupu zenye maudhui machafu kimaadili kinyume na Sheria pamoja na kifaa cha
kielektroniki ambacho alikuwa akitumia kusambaza picha hizo chafu.
Akizungumza na vyombo vya habari Kamanda wa Polisi mkoani
Pwani Salim Moracase amesema walimnasa mtu huyo baada ya kupokea taarifa kutoka
kwa uongozi wa Shule ya Baobab, iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani, kuwapo kwa watu waliotengeneza
picha walizoziuganisha na baadhi ya majengo ya shule ili kuaminisha umma kuwa
vitendo hivyo vinafanyika shuleni hapo.
Jeshi la polisi limefanya uchunguzi limefanikiwa
kumkamata mtu mmoja ambaye uchunguzi wa kitaalamu ulisaidia kumfikia na kumkuta
na picha hizo na kifaa ambacho alikuwa akitumia kusambaza picha hizo chafu,
amesema Kamanda Moracase.
Aidha, Kamanda Moracase amesema polisi bado wanaendelea
kuwasaka watu wengine waliohusika katika kutengenezea na kusambaza picha hizo.
Jeshi hilo limetoa onyo kwa watu wenye tabia kama hizo za
kutengengeneza picha kama hizo kwa malengo ya kuchafua wengine au taasisi kwani
mkono wa sheria lazima utawafikia.
0 Maoni