WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amewataka wafamasia nchini watoe dawa kwa kuzingatia maadili ya
taaluma yao na waache kutoa dawa kiholela ili kuimarisha ufanisi wa huduma za
afya na kuwalinda wananchi dhidi ya madhara yatokanayo na matumizi ya dawa
yasiyo sahihi.
Ameyasema
hayo leo (Jumatano, Desemba 4, 2024) alipofungua Kongamano la Kisayansi na
Mkutano Mkuu wa 54 wa Chama cha Wafamasia Tanzania, ambapo amewataka watumie
ujuzi na utaalamu wao kuwapa wahitaji dawa sahihi na kwa kuzingatia vipimo na
maelekezo ya Madaktari.
“Watanzania
wenzangu, wakati umefika wa kuacha kutumia dawa pasipo ushauri wa watalamu wa
afya. Nendeni katika vituo vya kutolea huduma za afya mpate vipimo na maelekezo
sahihi ya matumizi ya dawa. Pia Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba simamieni
matumizi sahihi ya dawa hasa za antibiotics.”
Waziri Mkuu
ameongeza kuwa suala hilo liende sambamba na kusimamia vizuri huduma za utoaji
dawa katika maduka ya dawa na kuhakikisha madhara yanayoweza kutokea kutokana
na matumizi ya dawa na vifaa tiba yanadhibitiwa kwa ukaribu.
Aidha,
Waziri Mkuu ameitaka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba iongeze udhibiti wa upotevu
wa dawa, hususan kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vya umma. “Wizara ya
Afya pamoja na TAMISEMI tumieni mifumo iliyopo katika kuziba mianya ya upotevu
dawa vituoni na upatikanaji wa maoteo sahihi ya dawa ili kuepuka dawa
kuharibika.”
Kadhalika,
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutaja jitihada zinazofanywa na Serikali katika
kuimarisha huduma za dawa kuwa ni pamoja na kuendelea kutoa fedha kiasi cha
shilingi bilioni 16 kila mwezi kwa ajili
ya dawa. “Hatua hiyo imeimarisha
upatikanaji wa dawa hadi umefikia wastani wa asilimia 85.”
Waziri Mkuu
amesema Serikali katika kuhakikisha nchi inaimarisha uwezo wa uzalishaji wa
dawa na bidhaa nyingine za afya, imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji
ambapo kwa sasa kuna viwanda 17 vya dawa, 75 vya vifaa tiba na viwanda 57 vya
kutengeneza gesitiba.
Katika hatua
nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ameitaka Wizara ya Afya na Bohari Kuu ya Dawa
kuiangalia upya sheria ya uagizaji wa dawa nchini kama inakidhi mahitaji ya
sasa kwa kuwa inataka kutumia muagizaji mmoja.
“Ninataka
mje mnishawishi ni kwanini tusiipeleke Sheria hii bungeni tuibadilishe ili tuwe
na waagizaji zaidi ya mmoja, kwa kuwa tunakwenda kuanzisha Bima ya Afya kwa
Wote tunahitaji dawa mpaka zahanati, tunahitaji dawa za kutosha, hivyo muagizaji
mmoja hatatosha.”
Kwa upande,
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amewataka wafamasia wahakikishe
wanapotumia vyeti vyao katika uanzishwaji wa maduka ya dawa wabaki kufanyakazi
katika maduka hayo ili kuwezesha usimamizi mzuri badala ya kuweka vyeti na
kuondoka.
Awali, Rais
wa Chama cha Wafamasia Tanzania, Mfamasia Fadhili Hesekiah alitumia fursa hiyo
kumshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha mazingira ya
uwekezaji katika sekta mbalimbali nchini ikiwe ya afya.
0 Maoni