Jaji Warioba atahadharisha polisi kuingizwa kwenye siasa

 

Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba, ametahadharisha hatua ya Jeshi la Polisi kuanza kuingizwa kwenye siasa, na kuonya kuwa kitendo hicho ni hatari kinaweza kuwagawa wananchi.

Jani Mstaafu Warioba ametoa kauli hiyo leo Desemba 4, 2024 alipozungumza na Wahariri na Waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, na kusisitiza vyombo vya dola visiingizwe kwenye mambo ya siasa.

“Katika miaka michache iliyopita tumeliingiza Jeshi la Polisi kwenye siasa, na jeshi nalo limekuwa linatoa matamko ya kisiasa na hii italeta mgawanyiko,” alisema Jaji Mstaafu na kuongeza,

“Wananchi watagawanyika. Kuna wale watakaoona, Jeshi la Polisi ni adui, tusifike huko. Tuliache Jeshi la Polisi lifanye kazi zake za kawaida.”

Amesema kwamba sasa hivi inapofika wakati wa uchaguzi vyombo vya dola vinaandaliwa kwa ajili ya kukabiliana na ghasi, “Uchaguzi sasa umekuwa kama jambo la hatari, haipaswi kuwa hivyo.”

Jaji Mstaafu Warioba ambaye alikuwa akitoa maoni yake kuhusu uchaguzi wa serikali za mitaa uliomalizika, amesema kuwa ulikuwa na kasoro na kasoro hizo zinapaswa kurekebishwa.

“Uchaguzi huu umeharibiwa na wasimamizi ambao waliwawekea mapingamizi wagombea jambo ambalo ni kinyume, kwani wanaopaswa kuwekeana mapingamizi ni wagombea wenyewe,” alisema Jaji Mstaafu Warioba.

Pia, amedai kuwa wasimamizi wa uchaguzi walishiriki katika kuweka kura feki na cha kushangaza hadi sasa Serikali imekaa kimya haijawachukulia hatu watu walioshiriki kuharibu uchaguzi.

“Zamani waliokuwa wakishiriki kuandaa kura feki walikuwa wagombea, ajabu sasa hivi wanaoshiriki kuandaa kura feki ni wasimamizi wa uchaguzi,” alisema Jaji Mstaafu Warioba akionyesha kushangaa.



Chapisha Maoni

0 Maoni